Na nyinyi Waumini, pale mnapo washinda, na mkawauwa mlio wauwa katika wao, basi hakika si nyinyi mlio wauwa kwa nguvu zenu, lakini ni Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliye kupeni ushindi na kuweza kuwauwa, kwa msaada wake kwenu na kutia khofu katika nyoyo zao. Na wewe Mtume, pale ulipo warushia mchanga na kokoto nyusoni mwao kuwafazaisha, si wewe ulio rusha, lakini ni Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliye rusha, na wao wakafazaika. Na hayo Mwenyezi Mungu ameyafanya kuwaneemesha Waumini kwa neema njema. Katika hayo pana majaribio ya nguvu kwao, ili ionekane ikhlasi yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua mambo yao, Mwenye kusikia maneno yao, na Mwenye kujua mambo ya maadui zao na kauli zao pia.
Ikiwa nyinyi washirikina mlikuwa mkining'inia mapazia ya Al Kaaba na huku mnaomba yapambanuliwe baina yenu na Waumini ijuulikane haki ipo wapi, basi sasa imekwisha kujieni hukumu ya kupambanua, na ushindi si wenu, bali ni wa Waumini. Na nyinyi mkirejea tena kufanya uadui Nasi tutakushindeni tena. Wala kukusanyika kwenu kwa ajili ya madhambi hakutakufaeni kitu! Hata ikiwa idadi yenu kubwa vipi! Kwani hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao isaidiki Haki na wanaikubali.
Enyi mlio isadiki Haki, na mkaifuata! Hakika mmejua ushindi umepatikana kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na kumt'ii Mtume wake. Basi endeleeni kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume. Wala msiupuuze wito wa Mtume anao itia Haki, nanyi mnamsikia na mnafahamu ayasemayo.
Hao washirikina na wanaafiki ni kama wanyama waovu kabisa walio sibiwa na uziwi, kwa hivyo hawasikii; na wakasibiwa na ububu, kwa hivyo hawasemi. Basi wao ni viziwi kwa Haki, na hivyo hawasikii, wala hawaitamki na hawaielewi!!
Na Mwenyezi Mungu kwa ilimu yake ya tangu na tangu lau angeli ona ndani yao kuwa, katika hali yao hivi sasa, itakuja patikana kheri yoyote kwao hao kwa nafsi zao, na kwa watu, na kwa Haki, basi angeli wafanya wasikie kusikia kwa kuongoka hata Haki ikaingia akilini mwao. Na hata wangeli isikia na wakaifahamu Haki basi bado wasingeli ifuata. Na mapuuza hayawaachi kwa kuzidiwa na pumbao.
Enyi mlio isadiki Haki na mkaifuata! Muitikieni Mwenyezi Mungu kwa kufikisha anayo kuamrisheni. Na muitikieni Mtume katika vile anavyo fikisha anayo yaamrisha Mwenyezi Mungu, pale anapo kuiteni Mtume kufuata amri za Mwenyezi Mungu ambazo zitakuleteeni uzima wa miili yenu, na roho zenu, na akili zenu, na nyoyo zenu. Na mjue kwa yakini kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenya kuangalia nyoyo zenu. Huzielekeza atakavyo. Basi Yeye huingilia baina yenu na nyoyo zenu zinapo ingiliwa na matamanio, Yeye basi hukuokoeni nayo ikiwa nyinyi wenyewe mnajielekeza kwenye Njia iliyo nyooka. Na nyinyi nyote mtakusanywa kwake Siku ya Kiyama, na huko ndiko malipo yatakuwa.
Na jikingeni na Dhambi kubwa ya kufisidi jamii yenu, kama vile kuacha kwenda kwenye Jihadi, na kufarikiana mkagawana mapande mapande, na kama kuacha kuamrisha mema na kukataza maovu. Kwani Fitna hiyo, Dhambi hiyo, haiwapati wale walio dhulumu peke yao, bali inawapata wote. Na mjue kuwa bila ya shaka kuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali hapa duniani na Akhera pia.