Ewe Nabii! Waambie hao mateka walio angukia mikononi mwenu: Ikiwa katika nyoyo zenu ipo kheri anayo ijua Mwenyezi Mungu, Yeye atakulipeni yaliyo bora zaidi kuliko hicho walicho kichukua Waumini, na atakusameheni ushirikina wenu na madhambi mliyo kuwa nayo. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghfira na rehema kwa mwenye kutubia madhambi yake.
Na pindi wakitaka kukukhuni, kwa vile baadhi yao walivyo onyesha kumili kwenye Uislamu, pamoja na nyoyo zao kupenda kukufanyia khiana makusudi, wewe usivunjike moyo. Mwenyezi Mungu atakupa uwezo juu yao. Kama hapo kwanza walipo mkhini Mwenyezi Mungu kwa kumfanyia wenzi na washirika wa kuwaabudu, na wakaikufuru neema yake, na Yeye aliwaweza kwa kukupa ushindi juu yao katika Badri, juu ya kuwa jeshi lako ni dogo na lao ni kubwa. Na Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye ushindi, Muendeshaji kwa hikima yake, aliwathibitisha wakawa na nguvu waja wake Waumini kwa nusura yake.
Hakika walio isadiki Haki na wakaikubali hukumu yake, wakahama Makka, wakapigana Jihadi kwa mali yao na roho zao, na wale walio wapa makaazi wakimbizi ugenini, wakamsaidia Mtume wa Mwenyezi Mungu, wanapigana vita na wale wanao wapiga vita. Wanamfanyia uadui anao wafanyia uadui. Wao kwa wao wanasaidia kuunga mkono Haki, na kutukuza Neno la Mwenyezi Mungu. Na wale wasio hama, haijathibiti kupata ulinzi na msaada wa Waumini, mpaka wahajiri. Lakini wakikutakeni muwanusuru na wanao wakandamiza katika Dini, basi wanusuruni. Wakikutakeni muwasaidie dhidi ya watu ambao mna mapatano nao, na wala hawakuvunja mapatano hayo, basi msiwakubalie. Na Mwenyezi Mungu anayaona myatendayo, hana kinacho fichika kwake. Basi simameni kwenye mipaka yake msije mkatumbukia katika adhabu yake.
Na walio kufuru wao ni marafiki wenyewe kwa wenyewe. Na wao husaidiana kwa mambo ya upotovu, na wanaungana mkono kukufanyieni nyinyi uadui. Basi nyinyi msifanye nao urafiki. Mkikhaalifu, yaani mkenda kinyume na haya mkawafanya ni wenzenu itaingia fitna katika safu zenu, na utakuwa uharibifu mkubwa katika nchi.
Na walio amini, na wakahajiri, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na walio wapa makaazi, na wakaisaidia Haki na Neno la Mwenyezi Mungu - hao ndio walio na Imani ya kweli. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu atawasamehe, na watapata riziki kubwa duniani na Akhera.
Na walio amini baada ya wale wa mwanzo, na mwishoe wakahama nao, na wakapigana Jihadi pamoja na walio tangulia, basi hao ni katika nyinyi, kwa mkusanyiko wa Muhaajirina (Walio hama Makka) na Ansari (walio msaidia Mtume, watu wa Madina). Hao wanastahiki ulinzi na haki kama ziliopo baina ya nyinyi kwa nyinyi. Na walio kuwa wame nasibiana katika Waumini - juu ya urafiki wa Imani -wana urafiki zaidi wa kuwa ni jamaa. Basi hao wanazidiana katika mapenzi, na mali, na kusaidiana, na kuungana mkono. Na Mwenyezi Mungu ameyabainisha hayo katika Kitabu chake. Naye ni Mwenye kujua kila kitu.