Na enyi Waumini! Kumbukeni nanyi mnagawana ngawira na mnakhitalifiana, mlipo omba uwokovu na msaada, na mkaandikiwa kuwa hapana la kukuepusheni na vita. Mwenyezi Mungu alikuitikieni maombi yenu, akakuungeni mkono kwa kukuleteeni (Malaika) Roho zilizo safi nyingi zinazo fika elfu zinazo fuatana, zikija moja baada ya moja. Walipo jua wapiganaji Waumini kuwa hapana njia ya kuepukana na vita wakaomba msaada kwa Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu Mtukufu akawaitikia, na akawaunga mkono kwa Malaika elfu walio fuatana. Yaani alianza kwa kupeleka msaada kwa vikosi vilivyo fuatana ili iwe wepesi kwa kila kikosi kuelekea pahala pake katika vita pasiwepo kukaa bure au kupigana makumbo. Na ifikapo misaada ya majeshi ya vita roho hufurahi na moyo huingia nguvu. Na hayo ndiyo aliyo yakusudia Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kauli yake: "Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara na ili nyoyo zenu zituwe." Na ushindi daima unatokana na Mwenyezi Mungu.
Wala Mwenyezi Mungu Mtukufu hakujaalia huko kukuungeni mkono kwa (Malaika) hizo Roho safi ila ni kuwa ni kukupeni khabari njema, kama bishara kwenu kuwa mtashinda, mpate kutua nyoyo na msonge mbele. Na Mwenyezi Mungu anakusaidieni, na wala ushindi hauji ila kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye kushinda, ambaye anaye panga mambo kwa pahala pake kwa mujibu wa ujuzi wake usio pitikiwa na chochote.
Enyi Waumini! Kumbukeni wakati mlipo ingiwa khofu kwa upungufu wa maji, na kuwaogopa maadui. Mwenyezi Mungu alikupeni utulivu, kwa kukuleteeni usingizi, mkalala mkatua. Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni mkajisafishia, na mkauondoa wasiwasi wa Shetani, na nyoyo zenu zikawa imara kwa msaada wa Rahmani na pia ardhi ikashikamana kwa hayo maji, na miguu yenu ikaweza kukanyaga bila ya kudidimia katika mchanga. Aya hii inaashiria fadhila ya Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya wapiganaji Waumini kwa kupatikana hali ya amani kwa kupumzika kwa usingizi, na kuteremka mvua kwa kujitahirisha na kukoga, na kushikamana mchanga kwa kuwepo maji, basi nyayo zikasimama imara. Inajuulikana kuwa mchanga laini unawaletea taabu wapiganaji na unakuwa pingamizi katika kwenda huku na huko ambako ni katika dharura za vita muhimu. Na aya ya pili inaeleza maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaambia Malaika wawathibitishe Waumini na watie khofu katika nyoyo za makafiri. Na ni maarufu kuwa khofu ikiwatawala askari katika midani huwaletea kuemewa. Na katika Aya hii tukufu panaashiriwa pahali pa kupiga napo ni juu ya shingo na kuvikata vidole vinavyo kamata silaha mkononi.
Enyi Waumini! Kumbukeni pale Mwenyezi Mungu alipo wafunulia wale wenye Roho zilio t'ahirika, yaani Malaika, watie ndani ya nyoyo zenu kuwa Mimi ni pamoja nanyi, nakuungeni mkono, na ninakusaidieni, kwa kuwaambia: Zitieni nguvu nyoyo za walio amini, wait'ii Haki na wapigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Na Mimi nitaifanya khofu izitawale nyoyo za washirikina, nao watakuogopeni. Nanyi enyi Waumini! Wapigeni vichwani mwao vilio juu ya shingo zao, na kateni vidole vyao vinavyo kamata panga.
Ukawa ushindi na kuungwa mkono nyinyi, na kwao ni kitisho na fazaa, kwani wao walikuwa upande mmoja, na Mwenyezi Mungu na Mtume wake walikuwa upande mwengine, kwa kuwa wao walimpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi ndio Mwenyezi Mungu anawateremshia adhabu chungu. Na adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.
Enyi Waumini! Hivyo ndio vita, basi vionjeni, na muwe na yakini kuwa mtapata nusura na kuungwa mkono. Na wanao pinga Ishara za Mwenyezi Mungu watapata adhabu nyengine Siku ya Kiyama, nayo ni adhabu ya Moto.
Enyi mlio isadiki Haki na mkait'ii! Mkikutana na wale walio kufuru katika uwanja wa vita nao wanakujieni kwa wingi wao, msiwakimbie mkazipa mgongo panga zao.
Na asiye wakaabili uso kwa uso, basi Mwenyezi Mungu amekasirika naye, na marejeo yake ni Motoni. Na huo ndio mwisho muovu kweli. Na mwenye kuacha kuwakaabili kwa kuwa ni hila na mbinu za vita, au kaacha kikosi kwenda jiunga na kikosi kingine cha Waumini apate kuwa na nguvu zaidi za mpambano, huyo hana dhambi.