Hakika hali yao iliyo sasa inaruhusu kuwaadhibu, kwani wanawazuia watu wasiutumie Msikiti ambao Mwenyezi Mungu ameutukuza kwa kuharimisha vita karibu yake. Lakini Mwenyezi Mungu anawaakhirisha kwa alivyo wakadiria katika ujuzi wake kuwa wengi wao watakuja amini. Wao wakati huu wa sasa sio walinzi wa kuunusuru huo Msikiti Mtukufu, bali wao wameunajisi kwa kutia ibada ya masanamu ndani yake. Ama wa kuunusuru hakika ni Waumini, wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu. Lakini wengi katika washirikina hawaijui Dini, wala hawajui cheo cha Nyumba hiyo Tukufu.
Na maombi yao kwenye Nyumba hii Tukufu (Al Kaaba) si chochote ila ni kupiga myunzi na makofi. Ilivyo kuwa hiyo ndiyo hali yenu, basi wacha mauti yakupateni, na yaonjeni katika uwanja wa vita, upate kubaidika (kuwa mbali) ushirikina kutokana na Al Kaaba. Na kuuliwa huko kwenu ni kwa sababu ya ukafiri wenu.
Hakika hao wanao zipinga Ishara za Mwenyezi Mungu na wanamshirikisha na miungu mingine, hutoa mali yao ili wawazuie watu wasiifuate Imani ya Haki! Nao wataendelea kutoa hayo mali, kisha hayo mali, kwa kuwapotea bure bila ya pato walitakalo, yatawaletea majuto na machungu. Na katika uwanja wa mpambano watashindwa hapa duniani, na kisha watakusanywa wote katika Jahannam, wakibaki na ukafiri wao.
Kwa kushindwa makafiri duniani na kuadhibiwa Motoni Akhera Mwenyezi Mungu anapambanua aliye khabithi wa roho na vitendo na maneno, awe mbali na aliye mwema wa roho yake na moyo wake. Na awafanye wale waovu makhabithi wapandane wenyewe kwa wenyewe, huyu juu ya huyu, na awatie Motoni Siku ya Kiyama. Na hao washirikina mafisadi ndio wenye kukhasiri peke yao, duniani na Akhera.
Hakika juu ya vitisho hivi, mlango wa matarajio ungali wazi. Basi ewe Nabii wa rehema! Waambie hawa wapinzani kuwa wakikoma, wakaacha inadi yao na ushirikina wao, basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atawasamehe vile vitendo vyao vilivyo kwisha pita. Na wakiendelea na upotovu wao, na wakarudia tena kukupigeni vita, basi mwendo wa Haki kwa walio tangulia umethibiti utakuwa ule ule, nao ni kuwa Haki lazima iushinde upotovu, pindi ikiwa wale watu wa Haki wakishika ut'iifu na njia za ushindi.
Na endeleeni kuwapiga vita washirikina mpaka waache kuharibu itikadi za Waumini kwa kuwatesa na kuwaudhi. Wakiacha ukafiri na kuwaudhi Waumini, na wakamsafia Dini Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvijua vitendo vyao, na atawalipa kwavyo.
Na wakiendelea na kupuuza kwao na kuwaudhi Waumini, basi enyi Waumini, jueni ya kuwa nyinyi mko katika ulinzi wa Mwenyezi Mungu, na huo ndio ulinzi wenye kupendeza na wenye nguvu kabisa. Na Yeye ndiye Mwenye kukunusuruni, na nusura yake ndio yenye nguvu zaidi na bora zaidi.