Na vyote viliomo Mbinguni na Ardhini ni vya Mwenyezi Mungu peke yake, ni vyake kwa kuviumba, na kuvimiliki, na kuvisarifu. Na marejeo ya mambo yao ni kwake Yeye. Kwa hivyo humlipa kila mmoja kama anavyo stahiki.
Nyinyi Umma wa Muhammad ni bora ya umati alio umba Mwenyezi Mungu kwa manufaa ya watu, maadamu mtaamrisha ut'iifu na mtakataza maasi, na mtakuwa ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu kwa Imani safi na ya kweli. Na lau kuwa Watu wa Kitabu wangeli kuwa ni wakweli katika imani yao kama nyinyi, basi ingeli kuwa ni bora kwao kuliko walivyo. Walakini baadhi yao ni Waumini, na wengi wao wameikiuka mipaka ya Imani na yanayo pasa.
Hao wapotovu hawawezi kukudhuruni nyinyi kama walivyo kuandalieni, wala hawakuathirini. Ijapo kuwa mtapata maudhi kwao, lakini athari yake haiselelei. Na hata wakipigana nanyi wataingia kiwewe wakimbie wasipambane nanyi, na hapo mwishoe hawatopata ushindi juu yenu maadamu nyinyi mtashikamana na kuamrisha mema na kukataza maovu.
Na Mwenyewe Subhana ameeleza kuwa lazima watapata madhila popote watapo kutikana, ila wakifungamana kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu na ahadi ya Waislamu. Na wao wamestahiki wapate ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na pia Mwenyezi Mungu amewajaalia lazima uwafikie unyonge na unyenyekevu kwa wengineo. Na hayo ni kwa sababu ya kukataa kwao Ishara zote za Mwenyezi Mungu zinazo onyesha Unabii wa Muhammad s.a.w. na vile kuridhi kwao hapo zamani kuuliwa Manabii ambako hakuwezi kuwa ni kwa haki, bali ni kwa uasi wao na uadui wao.
Watu wa Kitabu si wote sawa sawa. Miongoni mwao wapo walio simama msimamo mwema, wa uadilifu, wanakisoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu nyakati za usiku wakiswali.
Wanaamini kweli kuwepo Mwenyezi Mungu, na kuwa Yeye ni Mmoja tu. Wanaamini Mitume wote, hawamuabudu ila Mwenyezi Mungu. Na wanaamini kuwa itafika Siku ya Kiyama; wanaamrisha ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu, na wanakataza maasi, na wanawania kutenda mambo ya kheri. Hawa kwa Mwenyezi Mungu huhisabiwa miongoni mwa watenda wema.
Kheri yoyote wanayo ifanya watu hao hawatonyimwa thawabu zake. Na Mwenyezi Mungu amezizunguka kwa kuzijua na kuziweza hali zao na malipo yao.