Kisha Mwenyezi Mungu baada ya dhiki akakupeni neema ya utulivu, ambao ulidhihiri kwa usingizi ulio wafunika wale walio wa kweli katika Imani yao na kumtegemea kwao Mwenyezi Mungu. Ama kile kikundi kingine, hamu yao ni juu ya nafsi zao tu hawana jenginelo; kwa hivyo wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbovu za kijahiliya, wakisema kwa kuchukiwa: Tumepata ushindi wowote sisi huo tulio ahidiwa? Sema ewe Nabii: Mambo yote ya kushinda na kushindwa yako kwa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye mwenye kuyaendesha mambo kwa waja wake pindi wao wakichukua khatua za ushindi, au wakifanya mambo ya kusabibisha kushindwa. Na wao wanapo sema hayo wana jambo wanalo lificha katika nafsi zao, wala hawalidhihirishi. Kwani wao husema: Ingeli kuwa sisi tuna khiari yetu tusingeli toka, basi tusingeli shindwa. Waambie: Hata mngeli kuwa ndani ya majumba yenu na kama wapo walio andikiwa kuuliwa basi hapana shaka wangeli toka mpaka pahala pao pa kufa wakauliwa. Na Mwenyezi Mungu amefanya aliyo yafanya hapo Uhud kwa maslaha makubwa, ili apate kutoa ndani yenu ikhlasi, na azitahirishe nyoyo zenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua vilivyo yaliyo fichika ndani ya nyoyo zenu.
Enyi jamaa wa Kiislamu! Wale miongoni mwenu walio acha kusimama imara pale pahali pao walipo wekwa wasimame hakika ni Shetani ndiye aliye wavuta kwenye utelezi na kukosea kwa sababu ya makosa yao kumkhaalifu Mtume. Lakini Mwenyezi Mungu amekwisha wasamehe, kwani Yeye ni mwingi wa maghfira, na mwingi wa upole.
Enyi mlio amini! Msiwe kama walio kufuru wakasema, kwa mintarafu ya wenzao wanapo ondoka kwenda safarini kutafuta maisha wakafa, au wakenda vitani wakauwawa: Lau wangeli bakia nasi hapa wasingeli kufa, na wasingeli uwawa. Mwenyezi Mungu amejaalia kauli yao hiyo na dhana yao iwe ni majuto ya nyoyoni mwao. Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuhuisha na Mwenye kufisha, na kudra ya kila kitu imo mikononi mwake. Yeye anayajua yote myatendayo, ya kheri na shari. Na Yeye ndiye wa kukulipeni.
Na mkiuwawa katika Jihadi au mkafa wakati huo, basi hayo hakika ni kupata maghfira ya Mwenyezi Mungu kufutiwa dhambi zenu, na kupata rehema itokayo kwake. Hayo ni bora kuliko starehe za dunia ambazo mnge zikusanya lau mngeli bakia.