Ilikuwa ni rehema ya Mwenyezi Mungu kwako wewe (Muhammad) na kwao (Waumini) kwa kuwa wewe umekuwa laini kwao wala hukuwatolea neno la ukali kwa kukosea kwao. Na lau kuwa wewe ungeli kuwa unawachukulia kwa ukavu, na moyo mgumu wangeli kukimbia. Basi nawe yapuuze makosa yao, na waombee msamaha, na ushauriane nao katika mambo ili upate maoni yao katika mambo ambayo siyo ulio teremshiwa ufunuo, Wahyi. Ukisha funga azimio lako juu ya jambo baada ya kushauriana, basi endelea nalo na huku ukimtegemea Mwenyezi Mungu. Kwani Mwenyezi Mungu humpenda anaye mwakilisha mambo yake Yeye.
Mwenyezi Mungu akikuungeni mkono kwa nusura yake, kama ilivyo tokea siku ya Badri, hatokushindeni yeyote. Na akikuacheni mkono kwa kuwa nyinyi hamkuchukua khatua zifaazo za ushindi, kama yaliyo pita siku ya Uhud, basi hamtakuwa na wa kukunusuruni mwenginewe. Na ni juu ya Mwenyezi Mungu peke yake ndio yawapasa Waumini wategemeze mambo yao yote.
Haisihi kuwa Nabii yeyote kukhuni katika ngawira kama walivyo eneza kwa uzushi wanaafiki waongo. Kwani khiyana ni kinyume na Unabii. Basi isikupitikieni dhana hiyo. Na mwenye kukhuni atakuja Siku ya Kiyama na mzigo wa dhambi wa khiyana yake, tena kila nafsi italipwa ilicho tenda, kwa ukamilifu. Na wala hawatadhulumiwa kwa kupunguzwa thawabu zao wala kuzidishiwa adhabu yao.
Hawawezi kuwa sawa, anaye piga mbio kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu kwa vitendo na ut'iifu, na yule anaye stahiki ghadhabu kuu ya Mwenyezi Mungu kwa sababu ya uasi wake. Na mwenye kuasi ataishia Jahannamu, na kuovu kulioje huko!
Makundi mawili hayo hayawi sawa, bali yametafautiana mbele ya Mwenyezi Mungu kwa daraja mbali mbali. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zao na daraja zao, na atawalipa kwa mujibu wake.
Mwenyezi Mungu amewafadhili Waumini wale wa mwanzo walio kuwa na Nabii s.a.w. kwa kuwapelekea Mtume aliye tokana na wao wenyewe, akiwasomea Aya za Kitabu, na akiwat'ahirisha na itikadi mbovu, akiwafundisha Qur'ani na Sunna za Mtume, na ilhali kabla ya kuletwa Mtume, walikuwa katika ujinga na ubabaishi na upotovu.
Hivyo mnapigwa na mshangao na kuemewa pale yalipo kupateni siku ya Uhud masaibu ambayo nyinyi mlikwisha wapa maadui mara mbili mfano wa hayo katika siku ya Badri, hata mnasema kwa mastaajabu: Yamekuwaje mauwaji haya na kushindwa huku, na sisi ni Waislamu na Mtume wa Mwenyezi Mungu yuko nasi? Sema: Yaliyo kupateni yametokana na nafsi zenu kwa vile mlivyo mkhalifu Mtume. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, naye amekulipeni kwa mujibu wa mlivyo tenda.