Mwenye kumt'ii Mtume basi ndio amemt'ii Mwenyezi Mungu, kwani yeye haamrishi ila alicho amrisha Mwenyezi Mungu. Wala hakatazi ila alicho kataza Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo kumt'ii yeye (Mtume s.a.w.) ndio kutenda na kuacha kwa ut'iifu wa Mwenyezi Mungu. Na mwenye kukataa kukut'ii wewe basi, kwani Sisi hatukukupeleka wewe ila uwe ni mbashiri na mwonyaji tu, sio uwe ni mlinzi wao na muangalizi wao, uwalindie vitendo vyao. Hayo ni yetu Sisi sio yako.
Na kikundi hichi kinacho tapatapa husema: Amri yako tunait'ii. Hatuna kwako ila kut'ii unayo amrisha na kukataza. Lakini wakisha toka kwako wakawa mbali nawe, baadhi yao hupanga vijambo vyao usiku usiku, kinyume na unavyo waambia ya kuwaamrisha na kuwakataza. Na Mwenyezi Mungu, Subhanahu wa Taa'la, Aliye takasika na Kutukuka, anayadhibiti yote wanayo yapanga kwa siri. Basi usiwashughulikie, na wapuuze, na mwachie mambo yao Mwenyezi Mungu, na wewe mtegemee Yeye. Na Mwenyezi Mungu ni wa kutosha kuwa ni Mtegemewa wako, na Mlinzi wako wa kumwachilia mambo yako yote.
Basi hao wanaafiki hawakizingatii Kitabu cha Mwenyezi Mungu wakajua hoja za Mwenyezi Mungu zilio juu yao kuwa ni waajibu kut'ii na kufuata amri yako? Na kwamba Kitabu hichi kinatoka kwa Mwenyezi Mungu kwa yalivyo shikamana maana yake na hukumu zake, na kinavyo fungamana wenyewe kwa wenyewe? Hii ni dalili kuwa ni kweli kinatoka kwa Mwenyezi Mungu; kwani lau kuwa kinatokana na mwenginewe basi maana yake yangeli gongana, na hukumu zake zingeli khitalifiana sana.
Na hichi kikundi cha wanaafiki kikipata khabari zozote zilio khusu nguvu au udhaifu wa Waislamu huzitangaza na kuzieneza nje, ili kuwababaisha Waislamu au kuwatia khofu katika nyoyo zao, au ili zifike khabari zao kwa maadui wao. Na lau kuwa hawa wanaafiki watangazao wamerudisha jambo lilio kuhusu usalama au kitisho kwa Mtume na kwa wakuu wa mambo miongoni mwa waongozi na Masahaba wakubwa, wakataka kwao kujua hakika, wangeli jua hao wanao jitahidi kuchungua mambo na kuyatangaza, kuwa yaliyo kweli yanatokana na Mtume na waongozi wengine. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu kwa alivyo zithibitisha nyoyo zenu juu ya Imani, na kuzuia fitina, na rehema yake kwa kukupeni sababu na njia za ushindi, wengi wenu wangeli fuata upotovu wa Shetani, na wasingeli okoka kutokana na upotovu wake ila wachache tu.
Na kama wapo kati yenu mfano wa hawa wanaafiki basi wapuuzilie mbali. Na wewe pigana kwa ajili ya Neno la Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya Haki. Wewe huna jukumu ila la nafsi yako tu. Kisha waite Waumini wende vitani, na wahimize. Huenda Mwenyezi Mungu kwa kupitia kwako na kwao akazuia hayo mashambulio ya makafiri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukuungeni mkono, na ni Mwenye kukunusuruni. Na Yeye ana nguvu kuliko wote, na mkali kuliko wote katika kuwaadhibu makafiri.
Na hawa wanaafiki husaidia ufisadi, na watu wa Imani husaidia Haki. Na mwenye kusaidia jambo jema ana fungu lake la thawabu. Na mwenye kuwasaidia watu waovu naye ana mzigo wake wa dhambi katika malipo yake. Na Mwenyezi Mungu ana uweza juu ya kila kitu, na Mwenye kujua kila kitu.
Akikuamkieni mtu yeyote kwa maamkio ya salamu, au dua, au ya namna yoyote ya hishima, au namna nyengine yoyote ile, basi mjibuni kwa maamkio yaliyo mazuri zaidi, au kwa uchache mjibuni kama alivyo kuamkieni yeye. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kutia hisabuni kila kitu, kikubwa na kidogo.