Na lau kuwa Sisi tumewalazimisha mashaka ya mwisho, kwa kuwaamrisha wapigane Jihadi moja kwa moja, na wajitolee nafsi zao kutilifu, au watoke nje waache majumba yao kwenda pigana Jihadi daima, wasinge kubali kut'ii ila wachache tu. Lakini Mwenyezi Mungu, Aliye takasika na kutukuka, hakalifishi ila linalo wezekana. Na lau kuwa wange fanya hayo na wakafuata haki yake ingeli kuwa ni kheri yao ya duniani na Akhera. Na hivyo ndiyo inavyo pelekea kuthibiti Imani, na kuingia imara, na kuleta utulivu.
Na mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume kwa kuzifuata kwa unyenyekevu amri zao na kuridhia hukumu yao, basi huyo yu pamoja na alio waneemesha Mwenyezi Mungu kwa uwongofu na kuwawezesha duniani na Akhera. Na watu hao ni Manabii wake, na wafuasi wao walio wasadiki na kuwakubali na wakafuata nyendo zao, na Mashahidi walio kufa katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na watu wema watendao mema kwa siri na dhaahiri. Na hapana la kushinda uzuri kuliko kuwa pamoja na watu hawa - haingii mashakani mwenye kukaa nao, wala hayachoshi mazungumzo yao.
Hayo ni makao matukufu kwa mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hiyo ni fadhila kubwa inayo tokana na Mwenyezi Mungu. Naye anavijua sana vitendo vyenu, naye atakulipeni kwavyo. Yamtosha Muumini kuwa Mwenyezi Mungu anamjua, naye lake ni kumt'ii Mola wake Mlezi na kutafuta radhi zake.
Enyi Mlio amini! Daima kuweni na hadhari na maadui wenu. Jizatitini kupambana na vitimbi vyao. Na mkitoka kwenda vitani tokeni kwa vikosi vikosi, au tokeni nyote pamoja.
Na wahadharisheni wanao kaa nyuma wasende nanyi vitani. Miongoni mwa hao mnao ishi nao wakajizuia wasifuatane nanyi kwenda kupigana, mkipatwa na shida na masaibu katika Jihadi, wao wa kikundi hicho, kwa kufurahia yaliyo kusibuni, husema: Mwenyezi Mungu katufanyia kheri kwa kuwa hatukwenda nao vitani.
Na mnapo pata fadhila ya ushindi kutokana na Mwenyezi Mungu, mkapata ngawira za vita, kikundi hicho hicho, kwa kuona maya na kutamani, husema: Laiti tungeli kuwa nao katika vita hivi, nasi tukapata mafanikio ya ngawira nzuri. Na husema haya na hayo kama kwamba hapakuwepo mapenzi yoyote yaliyo wafunga wao na nyinyi.
Ikiwa yupo kati yenu anaye bakia nyuma asende kupigana kutokana na udhaifu wa Imani yake, au ulegevu wa azma yake, basi na wapigane, kuinua Neno la Mwenyezi Mungu na kuwania Haki, wale walio uza uhai wao wa dunia kutafuta uhai wa Akhera. Na mwenye kupigana vita kwa ajili ya kunyanyua Neno la Mwenyezi Mungu na kuwania Haki, atapata moja ya mema mawili. Ama atauliwa apate fadhila ya kufa shahidi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, au atashinda, apate fadhila ya kufuzu katika dunia. Naye katika hali zote mbili atapewa na Mwenyezi Mungu ujira mkubwa katika Akhera.