Uadilifu ndio nidhamu ya maumbile. Na hiyo ndiyo sharia ambayo haiwezi kuwapo ndani yake maoni ya kukhitalifiana. Basi enyi mlio mt'ii Mwenyezi Mungu wa Haki, na wito wa Mitume wake, kuweni macho nafsi zenu katika kuut'ii uadilifu, na kuweni macho kwa ajili ya watu. Mfanyieni insafu aliye dhulumiwa, na msimame imara, si kwa ajili ya kumpendelea tajiri, au kumwonea huruma masikini. Kwani Mwenyezi Mungu aliye waumba matajiri na masikini anastahiki zaidi kuangalia hali ya tajiri au fakiri. Matamanio ndiyo yanayo mpelekea mtu kumili nafsi yake, basi msiyafuate matamanio mkaacha uadilifu. Na mkikengeuka mkaacha uadilifu, au mkapuuza kusimamisha uadilifu, basi mjue Mwenyezi Mungu anayajua myatendayo, tena anayajua kwa ujuzi wa ndani. Naye atakulipeni kwa mujibu wa a'mali yenu; ikiwa njema mtalipwa wema, ikiwa ovu mtalipwa shari.
Kwa hakika Ujumbe wa mbinguni ni mmoja, kwa kuwa yule Mwenye kutuma ni Mmoja, naye ni Mwenyezi Mungu. Basi enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu na mumsafie niya. Na msadikini Mtume wake Muhammad, na msadiki yaliyo kuja katika Kitabu chake alicho mteremshia, na mtende yaliyo amrishwa humo. Na sadikini Vitabu vilivyo teremshwa kabla yake kama alivyo teremsha Mwenyezi Mungu bila ya mageuzo wala kusahau. Aminini yote hayo. Kwani mwenye kumkanusha Mwenyezi Mungu, Muumba wa viumbe vyote, na Malaika, na Mwenye kuyajua yaliyo fichikana, na Vitabu vya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na akaikanusha Siku ya Mwisho, basi huyo ameipotea Njia Iliyo Nyooka, na ametokomea mbali katika njia ya upotovu.
Hakika Imani ni kuit'ii Haki kusio kuwa na ukomo, na kunako endelea daima. Basi wanao taradadi wakababaika si Waumini. Hao ambao wanaamini, kisha wakakufuru, kisha wakaamini, kisha wakakufuru, na kwa hivyo wakazidi ukafiri wao - Mwenyezi Mungu hatakuwa wa kuwaghufiria watu hao hivyo vitendo vyao viovu, wala hatawaongoa kwenye Haki. Kwani kusamehe kwa Mwenyezi Mungu kunahitajia toba, na kujing'oa na shari, na uwongofu wake ni kwa wale wanao ielekea Haki na wanaitaka.
Hao wanaafiki huufanya utawala wa makafiri uwe juu yao, na wanawawacha Waumini. Basi hebu hivyo wanataka wapate utukufu kwa hawa makafiri? Hakika utukufu uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Yeye huwapa waja wake wenye kuamini. Na mwenye kutaka utukufu kwa Mwenyezi Mungu atatukuka, na mwenye kutaka utukufu kwa mwenginewe atadhalilika.
Mwenyezi Mungu amekwisha kuteremshieni katika Qur'ani Tukufu kwamba kila mkisikia Aya za Kitabu nyinyi mnaamini, na makafiri wanapinga na wanakejeli. Na ikiwa hivyo ndiyo hali ya makafiri na wanaafiki, na mkasikia kejeli zao, basi msikae nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine waache dhihaki zao. Na nyinyi ikiwa hamtofanya hivyo, mkawa mnasikiliza kejeli zao, basi mtakuwa nanyi kama wao katika kuifanyia maskhara Qur'ani. Mwisho wa makafiri na wanaafiki ni muovu mno, kwani Mwenyezi Mungu atawakusanya wote hao katika Moto wa Siku ya Kiyama.