Ewe Nabii! Huwastaajabii hao wanao dai kuwa wanasadiki Kitabu ulicho teremshiwa wewe na vilivyo teremshwa kabla yako wewe, wanataka wahukumiwe katika ugomvi wao kwenye upotovu na uharibifu na hukumu isiyo kuwa ya Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu amekwisha waamrisha wayapinge hayo, wala wasitake kuhukumiwa kwa hayo. Na Shetani anataka awaachishe Njia ya Haki na Uwongofu, awapotezelee mbali.
Na wakiambiwa: Njooni kwenye Qur'ani na Sharia aliyo iteremsha Mwenyezi Mungu, na njooni kwa Mtume wake akubainishieni, utaona hao wanaafiki wanajitenga nawe kabisa wanakukataa.
Itakuwaje hali basi yakiwateremkia masaibu kwa sababu ya uovu wao na upotovu wa vitendo vyao, na wasipate pa kukimbilia ila kwako! Hapo basi watakuapia Mungu mbele yako kuwa wao hawakukusudia kwa maneno yao na vitendo vyao ila wema tu na kutaka mapatano.
Hao ndio wanao kula yamini kuwa hawakutaka ila wema na vitendo vya muwafaka. Mwenyezi Mungu anayajua vyema yaliyomo katika nyoyo zao, na anaujua uwongo wa hiyo kauli yao. Basi wewe usishughulike na maneno yao. Waite kwenye haki kwa mawaidha yaliyo mema, na sema nao maneno yenye hikima yenye kuathiri yanayo fika ndani ya nyoyo zao.
Na Sisi hatukumtuma Mtume yeyote ila jambo lake kuu ni kuwa at'iiwe, na ut'iifu huo ni kwa ruhusa iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu. Na hakika mwenye kwenda kinyume, au kukanusha, au kukhaalifu, anakuwa ni mwenye kujidhulumu mwenyewe. Na lau kuwa hawa walio jidhulumu wakirejea kwenye uwongofu, wakakujia wakiomba msamaha kutokana na Mwenyezi Mungu kwa yale waliyo yatenda, na wewe ukawaombea msamaha kwa mujibu wa ujumbe wako na kwa ulivyo ona ilivyo geuka hali yao, basi hapana shaka watamkuta Mwenyezi Mungu, Aliye takasika na kutukuka, ni Mwingi wa kukubali toba, na Mwenye kuwarehemu waja wake.
Naapa kwa jina la Mola wako Mlezi! Hawahisabiwi kuwa ni Waumini wa Haki na wenye kuinyenyekea, mpaka watakapo kufanya wewe hakimu muamuzi wa mizozo inayo tokea baina yao. Kisha nafsi zao zisione dhiki kwa utavyo hukumu, na wakunyenyekee kama wanavyo nyenyekea Waumini wa kweli.