Hakika Mwenyezi Mungu aliye kuteremshia Qur'ani na akakulazimisha uifikishe kwa watu na ushikane nayo hapana shaka atakurudisha kwenye miadi, nako ni Siku ya Kiyama, ili apambanue baina yako na wale wanao kukadhibisha. Ewe Mtume! Waambie makafiri: Mola wangu Mlezi ndiye anaye jua kwa ujuzi usio pikuliwa na yeyote, nani aliye mpa uwongofu na uwongozi, na nani aliye tumbukia katika upotovu unao tambulikana na kila mwenye akili nzima.
Ewe Mtume! Wewe hukuwa wewe ukitaraji na ukingojea uteremshiwe hii Qur'ani. Lakini Mwenyezi Mungu amekuteremshia kutoka kwake kwa kukurehemu wewe na umma wako. Basi ikumbuke neema hii, na shikilia kuifikisha. Wala usiwe wewe na wanao kufuata kuwa wasaidizi wa makafiri kwa wanayo yataka.
Wala makafiri wasikuachishe kuzifikisha Aya za Mwenyezi Mungu na kuzitenda, baada ya kwisha teremka wahyi (ufunuo) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na ukawa ndio Ujumbe wako. Na shikilia Wito kuwaitia watu kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu. Wala usiwe wewe wala wanao kufuata katika wasaidizi wa washirikina kwa kuwasaidia kwa wayatakayo.
Wala usimwabudu mungu yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu tu. Kwani hapana kabisa mungu wa kuabudiwa kwa haki isipo kuwa Yeye. Kila kitu isipo kuwa Mwenyezi Mungu kitaangamia na kwisha. Wa kudumu milele ni Yeye Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye mwenye hukumu ya kutekeleza duniani na Akhera. Na kwake Yeye ndiyo yako marejeo ya viumbe vyote, hapana hivi wala hivi.