Alipo elekea Madyana, kijiji cha Shuaibu - kwa kuwa huko iko amani - alimwomba Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu amwongoe njia ya kheri na ya kuokoka.
Alipo yafikia maji ya Madyana wanapo nyweshea maji alikuta karibu na kisima kundi la watu wengi mbali mbali wanawanywesha wanyama wao wa mifugo. Na pahali pa chini kuliko hapo pao akawakuta wanawake wawili wanawazuia kunywa maji kondoo na mbuzi wao. Musa akawaambia: Mbona mko mbali na maji? Wakajibu: Hatuwezi kusukumana, na wala hatunyweshi sisi mpaka hawa wachunga wamalize wao kunywesha. Na baba yetu ni mkongwe, hawezi kuchunga wala kunywesha wanyama.
Musa akajitolea kuwakhudumia akawanyweshea. Kisha akenda kuegemea mti akipumzika baada ya kuhangaika kule, naye akisema kwa unyenyekevu: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika mimi ni mwenye haja ya kheri yoyote na riziki yoyote utayo niletea.
Mmmoja wa wale mabinti akaja na ujumbe kutoka kwa baba yake baada ya kwisha jua khabari za Musa na wao wale mabinti. Naye akaja na huku anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita ili akulipe ujira kwa ulivyo tunyweshea maji. Basi alipo kwenda kwake na akamsimulia kisa chake cha kutoka Misri, akasema yule mzazi wa mabinti: Usikhofu; umekwisha okoka kwa hao watu madhaalimu. Kwani Firauni hana madaraka juu yetu.
Mmoja wa wale mabinti alisema: Ewe baba yangu! Mchukue umpe kazi ya kuchunga kondoo na mbuzi na kuwasimamia kwa haja zao. Hakika huyu ni mbora wa kumuajiri kwa sababu ya nguvu zake na uaminifu wake.
Shuaibu a.s. akamwambia: Mimi nataka kukuoza mmoja wa hawa mabinti zangu kwa mahari ya kunifanyia kazi muda wa miaka minane. Ukitimiza kumi itakuwa ni khiari yako. Wala mimi sitaki kukulazimisha huo muda mrefu. Na Inshallah, Mwenyezi Mungu akipenda, utaniona mimi ni katika watu wema, wenye kwenda nawe kwa ihsani na kutimiza ahadi.
Musa akasema: Hayo uliyo niahidi ni sawa sawa baina yangu na wewe. Muda wowote katika huo nitakao kufanyia kazi itakuwa nimekutimizia ahadi yako. Wala mimi sitaki zaidi kuliko hayo. Na Mwenyezi Mungu ni shahidi kwa tunayo yasema.