Na tuwathibitishe katika nchi, na wawe na pahali pao humo. Na tuwathibitishie Firauni na Hamana na majeshi yao yale waliyo kuwa wakiyakhofu, nayo ni kuondoka ufalme wake kwa mkono wa mwenye kuzaliwa katika Wana wa Israili.
Na Mwenyezi Mungu alimfahamisha mama yake Musa, alipo kuwa anamkhofia asichinjwe na Firauni kama alivyo kuwa akiwachinja watoto wanaume wa Bani Israili, kwamba amnyonyeshe kwa kituo na hatauliwa na Firauni. Ikiwa anaogopa asije kutambulikana amtie katika sanduku, na amtie katika mto wa Nile bila ya khofu wala huzuni. Kwani bila ya shaka Mwenyezi Mungu amedhamini kumhifadhi na kumrejeshea mwenyewe, na kumtuma kwa Wana wa Israili.
Watu wa Firauni wakamchukua, ili aliyo kadiria Mwenyezi Mungu yatimie, yaani Musa apate kuwa Mtume mwenye kuwapinga wao, na mwenye kuwaletea huzuni, kwa kuitoa kombo dini yao na kuishambulia dhulma yao. Hakika Firauni na Hamana na wasaidizi wao walikuwa ni watu wenye madhambi, walio pindukia mipaka katika ujeuri na uharibifu.
Mke wa Firauni alipo mwona mtoto alimwambia mumewe: Mtoto huyu atatuletea furaha mimi na wewe. Tumweke, tusimuuwe, kwa kutaraji kuwa atakuja tufaa kuendesha mambo yetu. Au tumfanye mwenetu wa kumlea. Na wao kumbe hawatambui aliyo mkadiria Mwenyezi Mungu.
Na mama yake Musa akawa hajitambui kwa dhiki iliyo muingia kwa kuwa mwanawe kaangukia mikononi mwa Firauni. Akawa anakurubia kujitambulisha kwamba yeye ndiye mama yake. Lau ingeli kuwa Mwenyezi Mungu hakuutia imara moyo wake kwa kusubiri, basi angeli tangaza kuwa huyo ni mwanawe, jinsi alivyo kuwa akimhurumia, na pia ili awe miongoni mwa Waumini wenye kutulia.
Yule mama akamwambia dada yake Musa: Mfuatie upate kujua khabari zake. Basi akawa anamwona kwa mbali na anatahadhari asitambulikane, na Firauni na watu wake wakawa hawajui kama yule ni dada yake.
Mwenyezi Mungu alimjaalia yule mtoto akatae ziwa la kila mnyonyeshaji kabla hawajamjia mama yake. Watu wa Firauni wakaingiwa na ghamu, na wakashughulishwa na hayo. Yule dada yake ndio akawaambia: Nikuongozeni kwenye ukoo utakao muangalia huyu mtoto, na kumnyonyesha, na kumlea, nao watamtazama vizuri?
Wakaukubali uwongozi wake, na Mwenyezi Mungu akamrudisha kwa mama yake, ili nafsi yake itue, na afurahi kwa kurudi kwake, wala asihuzunike kwa kuwa mbali naye, na ili azidi kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyo mpa kuwa atamrudishia imetimia wala hayendi kinyume. Lakini watu wengi walikuwa hawajui kurudi Musa kwa mama yake, kwani hayo yote yalifichikana kwao.