Ewe Mtume! Aya hizi tunazo kufunulia wewe ni Aya za Qur'ani yenye kubainisha kwa uwazi, yenye kudhihirisha Haki iwe mbali na uwongo, na halali iwe mbali na haramu, na itoe ahadi ya kulipwa thawabu, na kuhadharisha na adhabu.
Hakika Firauni alipandwa na kiburi, na akapita mipaka katika udhalimu wake, na akatakabari mno katika nchi ya Misri. Akawafanya watu wa nchi hiyo makundi makundi, akiwanyanyua baadhi yao na akiwadhalilisha wenginewe, na khasa aliwadhoofisha Wana wa Israili. Akawa anawachinja watoto wao wanaume na akiwabakisha wanawake. Kwa hakika huyo alikuwa ni katika walio pita hadi katika ujabari na ufisadi.
Na Mwenyezi Mungu akataka kuwafadhilisha alio wafanya wanyonge Firauni katika nchi, na awafanye ndio wa kuongoza katika njia za kheri, na awarithishe ufalme na madaraka ya nchi.