Ewe Mtume! Sema: Enyi watu! Niambieni, Mwenyezi Mungu akikufanyieni usiku uendelee mfululizo bila ya mchana mpaka Siku ya Kiyama, je! Mnaye yeyote asiye kuwa Mwenyezi Mungu wa kukuleteeni mchana wenye mwangaza mkaweza kushughulikia maisha yenu na kuendesha mambo yenu ya dunia? Hamna hayo nyinyi. Basi kwa nini hamsikii kwa sikio la kuwaza na kuzingatia?
Ewe Mtume! Waambie watu: Mwenyezi Mungu akikujaalieni mchana mfululizo bila ya usiku mpaka Siku ya Kiyama, yupo asiye kuwa Mwenyezi Mungu wa kukuleteeni usiku mkapata kupumzika na kazi za mchana? Hamna hayo nyinyi. Basi kwa nini hamzioni Ishara za Mwenyezi Mungu, mkaamini na mkaongoka?
Na miongoni mwa rehema za Mwenyezi Mungu kwa viumbe vyake ni kuwa kawaumbia usiku na mchana, inayo fuatana, ili wapate kupumzika usiku, na washughulikie kutafuta riziki zao na manufaa yao mengine wakati wa mchana, na watambue fadhila za Mwenyezi Mungu juu yao wapate kumshukuru. "Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya usiku umekukalieni moja kwa moja, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu atakaye kuleteeni mwangaza? Basi je, hamsikii? Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya mchana umekukalieni moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu ataye kuleteeni usiku mkapumzika humo? Basi je, hamwoni? Na ni katika rehema zake amekufanyieni usiku na mchana mpate kupumzika humo na mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru." Hapana shaka kuwa kuumbwa kwa dunia kwa namna yake ilivyo sasa na ilivyo wekwa kwa mnasaba wa jua, na kuzunguka kwake wenyewe kwa wenyewe kila siku, na kulizunguka jua kila mwaka, hapana shaka kwamba haya yanaonyesha dhaahiri uwezo wa Mwenyezi Mungu na upweke wake. Na Aya tukufu inawazindua watu watambue ukweli ambao yawapasa wauelewe, nao ni kwamba Yeye Mtukufu lau kuwa aliumba dunia iwe na usiku wa milele, au iwe na mchana wa milele, basi hapanapo mungu mwengine anaye weza kuwaneemesha watu kwa mchana na usiku wa kufuatana kama hivi. Na hivyo ni kuwa lau kuwa dunia inazunguka juu ya msumari-kati wake na pia kulizunguka jua kwa kiwango kimoja kiasi ya siku 365 takriban, yangeli tokea mabadiliko makubwa mno. Miongoni mwao ni kudumu giza katika nusu ya dunia, na kudumu mwangaza katika nusu ya pili takriban. Na kwa hivi joto lingeli panda katika nusu yenye mwangaza kwa kiasi kisicho weza kuchukulika. Na nusu yenye giza ingeganda kwa barafu. Na pande zote mbili zisingeweza kuchukua kitu chochote chenye uhai. Ama huu mpango ulivyo sasa unapelekea kupishana usiku na mchana, na kwa hivyo kunapatikana mapumziko na utulivu wakati wa usiku, na kushughulika wakati wa mchana. Na hali ya hewa inasilihi uhai wa binaadamu, na wanyama, na mimea. Na haya ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu juu ya waja wake, ambazo zinapelekea tukubali uwezo wake, na tudumu kumshukuru.
Na pia, ewe Mtume, kumbuka siku watapo itwa washirikina na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa wito wa kuwatahayarisha, wakaambiwa: Wako wapi washirika ambao mkidai kuwa ni miungu wa kukunusuruni, au waombezi wa kukuombeeni?
Na Siku ya Kiyama tutatoa kutoka kila umma shahidi, naye ndiye Nabii wao, wa kutoa ushahidi dhidi yao kwa waliyo kuwa wakiyafanya duniani. Hapo Sisi tutawaambia wakhalifu miongoni mwao: Nini hoja yenu kwa mliyo kuwa mkiyatenda ya ushirikina na maasi? Watashindwa kujibu, na watajua hapo kuwa Haki yote iko kwa Mwenyezi Mungu, tangu mwanzo mpaka mwisho. Na yatapotea, kama vinavyo potea vitu vilio potea, yote waliyo kuwa wakimzulia Mwenyezi Mungu.
Sura hii inasimulia kisa cha Qaruni. Naye alikuwa katika kaumu ya Musa. Akapanda kiburi juu yao kwa kughurika kwa nafsi yake na mali yake. Na Mwenyezi Mungu alikuwa kampa khazina za mali mengi. Hata ikawa funguo zake tu zikiwaemea kundi la wanaume wenye nguvu! Na alipo ghurika na neema ya Mwenyezi Mungu juu yake, na akakufuru kwa sababu yake, watu walimpa nasaha, wakamwambia: Usidanganyike kwa mali yako, wala furaha kwa ajili yake isikusaliti hata ukaacha kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu hawapendi watu walio danganyika na wakasalitika. Na funzo la kisa hichi ni kuwa makafiri walio mkataa Muhammad s.a.w. walighurika na mali yao. Basi Qur'ani inawaelezea kuwa mali yao si chochote cha kutajika ukilinganisha na mali ya Qaruni.
Na katika utajiri na neema alizo kupa Mwenyezi Mungu toa fungu kwa ajili ya Njia ya Mwenyezi Mungu, na tenda a'mali kwa ajili ya makaazi ya Akhera. Na wala usiinyime nafsi yako fungu lake kwa matumizi ya halali katika dunia. Na wafanyie wema waja wa Mwenyezi Mungu, kama vile alivyo kufanyia wema wewe kwa neema zake. Wala usifanye uharibifu katika ardhi ukapita mipaka ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Subhanahu hawafurahii mafisadi kwa vitendo vyao viovu. Basi Qaruni hakusikia nasaha ya watu wake, na akasahau fadhila ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yake. Na akajifanya hajui kwamba Mwenyezi Mungu alikwisha waangamiza wengi walio mzidi yeye sana katika uwezo na mazoezi ya kuchuma mali kwa njia mbali mbali za uchumi. Na wakosefu hawaulizwi madhambi yao, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anayajua. Basi wataingizwa Motoni bila ya hisabu. Kuulizwa kwao ni kwa ajili ya kutahayarishwa tu.