Na lau kuwa vitu vyote viliomo duniani ni mali ya kila nafsi iliyo dhulumu kwa ushirikina na kukanusha, ingeli vitoa fidia kwa adhabu itayo wakabili Siku ya Kiyama, na ambayo wataviona vitisho vyake. Na hapo basi majuto na masikitiko yatawajaa nyoyoni mwao kwa kutoweza kuyatamka, na kwa fazaa itayo wapata kwa kuiona adhabu! Na hukumu ya Mwenyezi Mungu itapita juu yao kwa uadilifu, na wala hawatodhulumiwa katika malipo hayo, kwani hayo ni matokeo ya waliyo yatenda duniani!
Watu nawajue kuwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kumiliki na Mwenye madaraka makuu juu ya vyote viliomo mbinguni na duniani. Na pia wajue kuwa ahadi yake ni ya kweli. Basi Yeye hashindwi na kitu, na hapana yeyote ataye epuka malipwa yake. Lakini wao wamedanganyika na maisha ya dunia, hawajui hayo kwa ujuzi wa yakini!
Na Mwenyezi Mungu Subhanahu anavihuisha vitu baada ya kuwa havipo, na anaviondoa baada ya kuwapo. Na kwake Yeye tu ndio marejeo katika Akhera. Na mwenye kuwa hivyo hapana kuu la kumshinda.
Enyi watu! Kimekujieni kwa ulimi wa Mtume Muhammad Kitabu kilicho toka kwa Mwenyezi Mungu. Ndani yake mna makumbusho ya Imani, na ut'iifu, na mawaidha ya kuhimiza kheri, na kukataza vitendo viovu, na kueleza mzingatie khabari za walio kutangulieni, na kukutakeni muangalie utukufu wa uumbaji ili mpate kuuelewa utukufu wa Muumba. Na ndani ya Kitabu hicho mna dawa ya maradhi ya nyoyo zenu, maradhi ya shirki na unaafiki; na mna uwongofu wa kuendea Njia Iliyo Nyooka. Na yote hayo ni rehema kwa Waumini wanao itikia wito.
Ewe Mtume! Waambie: Furahieni fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu kwa kuiteremsha Qur'ani, na kubainisha Sharia ya Islamu. Na hii ni bora kuliko starehe zote anazo zikusanya mtu duniani, kwa sababu hichi ni chakula cha nyoyo na dawa ya maradhi yake.
Ewe Mtume! Waambie makafiri walio pewa baadhi ya starehe za duniani: Niambieni khabari ya vyakula vizuri vya halali alivyo kuruzukuni Mwenyezi Mungu, mkajifanya wenyewe ni watungaji sharia, mkahalalisha vingine na mkaharimisha vingine, bila ya kufuata Sharia ya Mwenyezi Mungu! Hakika Mwenyezi Mungu hakukupeni ruhusa mfanye hayo, bali nyinyi mnamzulia uwongo Mwenyezi Mungu.
Na watadhani nini Siku ya Kiyama hao walio mzulia uwongo Mwenyezi Mungu, wakajipa kuhalalisha na kuharimisha bila ya kuwa nayo dalili yoyote? Hakika Mwenyezi Mungu amewaneemesha neema nyingi na amezihalalisha kwao kwa fadhila yake, na amewawekea Sharia yenye kheri kwao. Lakini hawamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hayo, bali wanamzulia Mwenyezi Mungu uwongo!
Ewe Mtume! Hakika wewe umefikisha ujumbe wako, na hayo Mwenyezi Mungu anayajua. Na hapana jambo lolote katika mambo yako, na huwasomei Qur'ani, na wewe na umma wako hamtendi kitu, ila Sisi tunayashuhudia na tunayaangalia mnapo yaingia kwa juhudi. Na Mola wako Mlezi haachi kujua chochote hata kikiwa kina uzito wa chembe hichi, ikiwa katika mbingu au katika ardhi, kidogo na kikubwa. Vyote hivyo vinadhibitiwa katika Kitabu kilichoko kwa Mwenyezi Mungu, nacho ni chenye kubainisha wazi.