Wanao tenda mema kwa kuitikia Wito wa Mwenyezi Mungu, wakaamini na wakafanya kheri kwa Dini yao na dunia yao, hao watapata wema katika Akhera, na wema huo ni Pepo. Na tena watapata yaliyo zidi hayo kwa fadhila na ukarimu wa Mwenyezi Mungu. Wala nyuso zao hazitafunikwa na huzuni na hamu na fedheha. Hawa ndio watu wa Peponi watakao neemeka humo daima milele.
Na wale ambao hawakuitikia Wito wa Mwenyezi Mungu, wakakufuru, wakatenda maasi, watalipwa kwa mujibu ya uovu walio utenda. Na hawana mlinzi wa kuwakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na nyuso zao zitasawajika kwa ghamu na huzuni kama kwamba zimefunikwa na weusi wa kiza cha usiku! Na hao ndio watu wa Motoni, watasononeka humo milele.
Ewe Mtume! Kumbuka kitisho cha siku watapo kusanywa viumbe vyote, kisha tuwaambie walio mshirikisha Mwenyezi Mungu katika ibada zao: Simameni pahala penu nyinyi na hao mlio wafanya washirika wa Mwenyezi Mungu, muangalie mtafanywa nini? Patatokea mfarakano baina ya washirikina na hao miungu yao ya uwongo walio washirikisha na Mwenyezi Mungu. Hao miungu watajitenga na wale wafwasi wao, kwa kusema: Sisi hatukukutakeni mtuabudu. Wala nyinyi hamkuwa mkituabudu sisi! Hakika mlikuwa mkiyaabudu matamanio yenu tu!
Mwenyezi Mungu anatutosheleza kwa ilimu yake na hukumu yake kuwa ni Shahidi wa kutupambanua baina yetu na nyinyi. Sisi tulikuwa mbali nanyi, wala hatukuwa tunafaidika vyovyote kwa huko kutuabudu kwenu.
Katika msimamo huo kila mtu atajua kheri gani au shari gani aliyo ifanya, na atalipwa malipo yake. Na hapo hao washirikina watayakinika kuwa kweli Mwenyezi Mungu ni Mmoja na wa pekee, Mwenye Haki. Na yote waliyo kuwa wakimzulia Mwenyezi Mungu yatavunjika.
Ewe Mtume! Lingania kwenye Tawhidi safi, na useme: Nani anaye kuleteeni riziki kutoka mbinguni inapo teremka mvua, na katika ardhi inapo mea mimea na kuzaa? Na nani aliye kupeni kusikia na kuona? Na nani anaye toa vilio hai kutokana na vilio maiti, kama mimea, nayo ni hai kutokana na ardhi maiti? Nani anaye mtoa maiti kutokana na hai, kama mtu anavyo kufa? Na nani anaye panga na kuendesha mambo yote ya ulimwengu kwa kudra yake na hikima yake? Wataungama: Hapana pa kukimbilia! Kwa hakika ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mtenda yote. Ewe Mtume! Waambie watapo ungama: Si waajibu mkubwa kuit'ii Haki, na kumkhofu Mwenyezi Mungu, Mmiliki Ufalme wote?
Huyo basi ndiye Mwenyezi Mungu mliye mkiri, na Yeye tu peke yake ndiye Mola wenu Mlezi aliye thibiti kuwa ni Mola na Mlezi, na akapasa kuabudiwa pekee, wala hapana mwenginewe. Na hapana baada ya Haki ya Umoja wa Mwenyezi Mungu na kumuabudu Yeye tu, ila kutumbukia katika upotovu, nao ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kumuabudu mwenginewe. Basi vipi mnaiacha Haki mkauendea upotovu?
Kama ulivyo thibiti Ungu wa Mwenyezi Mungu na kumuabudu Yeye, vile vile imethibiti hukumu juu ya walio tokana na amri ya Mwenyezi Mungu wakimuasi kwa kuwa hawaifuati Haki. Kwani hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hawaongoi kwenye Haki ila wanao ishika njia yake, sio wanao mfanyia uasi.