Walipo hudhuria wachawi, na wakasimama mbele ya Musa kupambana naye kwa uchawi wao mbele ya watu, Musa aliwaambia: Leteni huo uchawi mlio nao!
Walipo tupa kamba zao na fimbo zao, Musa aliwaambia: Huo mlio fanya ni uchawi kweli, na Mwenyezi Mungu Subhanahu atauvunja kwa mkono wangu! Hakika Mwenyezi Mungu hawasahilishii mafisadi vitendo vyao vikawa vizuri na vyenye nafuu.
Ama Haki hapana shaka Mwenyezi Mungu atainusuru na ataiunga mkono kwa uwezo wake na hikima yake hata makafiri wakisaidiana katika kuichukia na kuipiga vita.
Na juu ya kudhihiri Ishara zote za kusadikisha Ujumbe, wale walio muamini Musa hawakuwa ila ni kikundi cha watu wachache tu katika kaumu ya Firauni. Waliamini juu ya kuwa wakiogopa asije Firauni na walio pamoja naye wakawaachisha waliyo yaamini. Jeuri za Firauni zilikuwa kubwa mno katika Misri! Hakika yeye ni katika walio pita upeo katika kutakabari na kujivuna.
Ama Musa aliwaambia Waumini kwa kuwawasa na kuwashajiisha: Enyi watu wangu! Ikiwa Imani imekwisha ingia nyoyoni mwenu kwa kumsafishia niya Mwenyezi Mungu, basi msimwogope yeyote mwenginewe. Nanyi msalimishie Yeye mambo yenu yote, na mtegemeeni Yeye, na muwe na yakini mwishoe atakunusuruni, ikiwa nyinyi mmethibiti katika Uislamu.
Waumini wakasema: Tunamtegemea Mwenyezi Mungu peke yake. Kisha wakamwomba Mola wao Mlezi asiwatie katika mitihani na mateso ya makafiri.
Tukawafunulia Musa na nduguye Haruni kuwapa amri wafanye nyumba za kukaa watu wao katika nchi ya Misri, na watu wa Imani wenye kufuata wito wa Mwenyezi Mungu wazielekee nyumba hizo, na wawe wanashika Swala kwa sura ya ukamilifu. Na Waumini wanabashiriwa kheri!
Walivyo shikilia makafiri katika kumfanyia inda Musa, alimwomba Mwenyezi Mungu kwa kusema: Ewe Mola Mlezi wangu! Hakika Wewe umempa Firauni na watukufu wake starehe za duniani, na mali, na wana, na utawala. Na matokeo ya neema hizi ni kupita kwao mipaka katika kupotea na kupoteza watu waache Njia ya Haki! Ewe Mwenyezi Mungu! Yafutilie mbali mali yao, na uwaache katika kiza cha nyoyo zao, wasijaaliwe kuipata Imani mpaka waione kwa macho adhabu iliyo chungu, ambayo ndiyo mwisho unao wangojea, ili wawe ni onyo kwa wengineo.