Na kila kitu mlicho ruzukiwa katika starehe za dunia na mapambo yake kina ukomo wake kwa muda mfupi. Hayo yasikuzuieni kuamini na kutenda vitendo vyema. Kwani hakika yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu huko Akhera, nayo ni thawabu na neema za milele, yana nafuu zaidi, na yana dawamu kuliko hayo yote. Basi kwa nini hamtumii akili zenu badala ya pumbao zenu?
Hawi sawa mwenye kuamini na akatenda mema na akastahiki ahadi ya Mwenyezi Mungu na ahadi ya malipo mema na Pepo, na akayapata kama alivyo muahidi Mwenyezi Mungu; kulingana huyu na yule aliye kanusha na akatenda vitendo viovu, na yakamzuga maisha ya dunia na mapambo yake, na kisha Siku ya Kiyama akawa katika walio hudhurishwa kwa ajili ya hisabu, na akawa katika wenye kuhiliki kwa adhabu.
Ewe Mtume! Kumbuka siku watapo simama hawa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuhisabiwa, naye Subhanahu akawaita kwa kuwatahayarisha: Wako wapi hao miungu mlio dai kuwa ni washirika wangu, wapate kukuteteeni na kukuombeeni?
Watasema waongozi wa makafiri katika walio stahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na vitisho vyake: Ewe Mola wetu Mlezi! Hawa tulio waita kwenye shirki na tukawapambia upotovu tuliwapoteza. Kwa sababu wao walikhiari ukafiri na wakaupokea, kama sisi tulivyo ukhiari na tukaupokea. Leo sisi tunajitenga nao kwako na ukafiri walio ukhiari duniani. Hawakuwa wao wakituabudu sisi; bali wakiabudu pumbao zao, na wakit'ii matamanio yao.
Na Mwenyezi Mungu kuwaamrisha makafiri ni kwa kuwatahayarisha tu, kwa vile kuwataka wawaite wale miungu ya ushirikina wawaokoe na adhabu yake, kama walivyo dai. Wakaitikia kwa unyonge, na wakawaita kwa kuwa hawana hila. Wasipate jawabu yoyote. Wakaiona adhabu walio ahidiwa iko mbele yao, na wakatamani lau kuwa katika dunia yao wangeli kuwa Waumini walio ongoka, jinsi ya adhabu iliyo wafikia.
Na ewe Mtume! Taja vile vile siku washirikina watapo itwa na Mwenyezi Mungu kwa kutahayarishwa, na wakaambiwa: Mliwajibu nini Mitume wangu nilio watuma kwenu wakuiteni kwenye Imani, nao wakafikisha Ujumbe?
Hii ndiyo hali ya washirikina. Ama mwenye kutubu kutokana na shirki yake, na akaamini Imani ya kweli, na akatenda mema, basi huyo hutaraji kuwa kwa Mwenyezi Mungu miongoni mwa walio fuzu kuipata radhi ya Mwenyezi Mungu, na neema ya kudumu yenye kuendelea milele.
Na Mola wako Mlezi anaumba atakalo kwa uwezo wake. Na anamkhitari amtakaye kwa hikima yake kumpa Ujumbe na ut'iifu kwa kujua kwake mwenyewe kufaa kwao. Wala hawawezi viumbe, na wala si haki, kumchagulia Mwenyezi Mungu walitakalo katika dini potovu, na miungu ya uwongo. Mtukufu ametakasika shani yake na washirika.
Ewe Mtume! Mola wako Mlezi anajua baraabara yaliomo katika vifua vya washirikina ya uadui wao juu yako, na wanayo tangaza kwa ndimi zao ya kukushutumu na kukupinga kwa ulivyo teuliwa kupewa Utume.
Na Mola wako Mlezi, ewe Mtume, ndiye Mwenyezi Mungu wa Haki, ndiye pekee Mwenye Ungu, Mwenye kustahiki peke yake kuhimidiwa na waja wake katika dunia kwa neema zake na uwongofu wake, na katika Akhera kwa uadilifu wake na kulipa kwake. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye hukumu, na kuamua baina ya waja wake. Na kwake Yeye ndiyo marejeo ya kwendea.