Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu amewateremshia Qur'ani kwa utungo, baadhi yake ikifuatia baadhi kwa mujibu wa inavyo takikana na hikima, na kulingana na ahadi, na maonyo, na hadithi, na mazingatio, ili wapate kupima na kuyaamini yaliomo ndani yake.
Wale ambao tuliwateremshia Taurati na Injili kabla ya kuteremka Qur'ani, na wakaviamini vitabu hivyo viwili, na wakasadiki yaliyo tajwa humo juu ya khabari za Muhammad na Kitabu chake, hao wanamuamini Muhammad na Kitabu chake.
Na hao wakisomewa Qur'ani hufanya haraka kutangaza Imani yao, na husema: Tumeyaamini hayo, kwani hayo ni Haki inayo toka kwa Mola wetu Mlezi; na sisi tulimjua Muhammad na Kitabu chake hata kabla ya kuteremka kwake, nasi tukanyenyekea kabla ya kusomwa kwake.
Hao ambao waliiamini Qur'ani na yaliyo teremshwa kabla yake, watapewa malipo yao maradufu - kwa ajili ya kuvumilia kwao mateso yaliyo wapata kwa ajili ya Imani, na wakakhiari vitendo vyema, na wakayakabili maovu kwa kusamehe na ihsani, na wakatoa katika njia ya kheri kutokana na mali aliyo wapa Mwenyezi Mungu.
Na wanapo sikia upotovu wa wajinga hujitenga mbali nao, kwa kujiepusha na kuondoka, na husema: Sisi tuna a'mali yetu na hatuiachi, na nyinyi mna a'mali yenu ya upotovu na madhambi yake yapo juu yenu. Na sisi tunakuacheni na mambo yenu, kwani sisi hatupendi kusuhubiana na majaahili.
Ewe Mtume! Hakika wewe una pupa sana kutaka hawa watu wako waongoke. Lakini wewe huwezi kumuingiza katika Uislamu kila umpendaye. Lakini Mwenyezi Mungu humwongoa kuendea Imani yule anaye mjua kuwa ameelekea uwongofu na ameukhiari. Na Yeye ndiye Mwenye kujua, wala hapana ajuaye zaidi kuliko Yeye, nani atakaye ingia katika safu za wenye kuongoka.
Na washirikina wa Makka walimwambia Mtume s.a.w. kwa kujitolea udhuru kwa kubakia kwao katika dini yao: Tukikufuata wewe katika dini yako Waarabu watatutoa katika nchi yetu, na watatushinda katika utawala wetu. Na hakika wao ni waongo katika kutoa udhuru wao huo. Kwani Mwenyezi Mungu alikuwa kawaweka imara na madhubuti katika nchi yao. Na akaifanya nchi takatifu yenye amani, hawashambuliwi wala hawauwawi, na hali wao ni makafiri. Na wanaletewa matunda na kheri nyengine za aina nyingi, ambazo Mwenyezi Mungu anawaletea kutoka kila upande. Basi huwaje awaondolee amani, na awaachilie wakinyakuliwa wakiongeza juu ya utakatifu wa Nyumba ya Alkaaba Imani kumuamini Muhammmad! Lakini wengi wao hawaijui Haki. Lau kuwa wanaijua wasinge khofu kunyakuliwa.
Watu hawa hawazingatii yaliyo wapata kaumu zilizo kwisha tangulia. Iliangamizwa miji ya walio ghurika na neema za Mwenyezi Mungu, na kisha wakazikanusha na wakamkanusha Mwenyezi Mungu. Na haya majumba yao yamekuwa matupu, magofu, hayafai kukaliwa ila nadra tu kwa wapita njia. Na yamebaki hayana mwenye kuyamiliki baada yao ila Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu na ukarimu.
Na haikuwa katika hikima ya Mwenyezi Mungu Mtukufu - naye ndiye Mola wako Mlezi aliye kuumba na kukuteuwa - kuiangamiza miji mikubwa ila baada ya kuwapelekea watu wake Mtume mwenye miujiza iliyo wazi awasomee Kitabu kilicho teremshwa, na awabainishie sharia, na kisha wawe hawaamini. Wala Sisi hatuangamizi miji mikubwa ila wakiwa watu wake wanaendelea na udhalimu na uadui.