Wala wewe Muhammad, hukuwa na Musa upande wa magharibi wa huo mlima, pale Mwenyezi Mungu alipo agana naye kumuamrisha Ujumbe. Wala hukuishi zama za Musa, wala hukushuhudia alipo fikisha Utume. Basi vipi hawa watu wako wanakanusha Utume wako na wewe unawasomea khabari za walio tangulia?
Na lakini Sisi tumeziumba kaumu nyingi katika vizazi vilivyo pitiwa na zama ndefu, hata wakasahau maagano yaliyo chukuliwa kwao. Na wewe, ewe Mtume, hukuwa mkaazi wa Madyana hata ndio uwasimulie watu wa Makka khabari zao. Lakini Sisi tumekutuma wewe, na tumekupa khabari zao kwa njia ya wahyi (Ufunuo).
Wala wewe, ewe Mtume, hukuwepo hapo kando ya mlima pale Mwenyezi Mungu alipo mwita Musa na akamteuwa kumpa Utume wake. Lakini Mwenyezi Mungu amekujuvya haya kwa njia ya wahyi (ufunuo), kutokana na rehema yake kwako na kwa umma wako, wapate kufikisha hayo kwa kaumu ambayo haikupata kufikiwa na Mtume kabla yako wewe, ili wakumbuke.
Ingeli kuwa makafiri wanapo patwa na mateso kwa sababu ya ukafiri wao wakataka udhuru na wakadai wakisema: Ewe Mola wetu Mlezi! Mbona hukutuletea Mtume tukamuamini na tukaikubali miujiza yake nasi tukawa miongoni mwa Waumini, basi usinge kuwepo Ujumbe wa Mitume.
Na alipo ileta Mtume wa Mwenyezi Mungu Qur'ani kutokana na Mwenyezi Mungu, makafiri walisema: Laiti yeye angeli pewa miujiza ya kuonekana na kama aliyo pewa Musa, na Kitabu cha kuteremka mara moja kama Taurati! Na hali hao walimkataa Musa na Ishara zake, kama hivi leo wanavyo mkataa Muhammad na Kitabu chake, na wakasema: Sisi tunawakataa wote wawili. Basi kukataa ndiko kuliko pelekea kuikanya miujiza.
Ewe Mtume! Waambie: Ikiwa hamuiamini Taurati na Qur'ani basi leteni kitabu kingine kinacho toka kwa Mwenyezi Mungu kilicho na uwongofu bora kuliko hivyo, au kama hivyo, nami nikifuate pamoja nanyi, ikiwa nyinyi mnasema kweli katika hayo madai yenu kwamba tuliyo kuja nayo ni uchawi.
Na ikiwa hawaitikii wito wako kwa kuleta kitabu kiongofu zaidi, basi jua kuwa wamebanwa na hawakubakiliwa na hoja yoyote, na kwamba kwa hayo wanafuata pumbao zao tu. Na hapana aliye zidi kwa upotovu kuliko yule anaye fuata pumbao lake katika dini, bila ya uwongofu kutokana na Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu hamwafiki mwenye kuidhulumu nafsi yake kwa kufuata upotovu bila ya kuitafuta Haki.