Wale walio amini, nao ni Manabii wa zamani, na Mayahudi, na Wakristo, na wanao tukuza nyota na malaika, na wanao uamini ujumbe wa Muhammad baada ya kuteuliwa kuwa ni Mtume, na wakaamini kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mmoja wa pekee, na wakaamini kuwa kupo kufufuliwa na kuhisabiwa Siku ya Kiyama, na wakatenda vitendo vyema duniani, basi watu hawa wana malipwa yao yaliyo wekewa kwa Mola wao Mlezi. Wala haitowapata khofu ya kuadhibiwa, na wala haitowafika huzuni kwa kukosa thawabu. Na Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa mwenye kutenda mema.
Kumbukeni pale tulipo chukua ahadi na agano juu yenu, tukaunyanyua mlima wa T'uur, tukaufanya kwa uwezo wetu kama kivuli juu yenu mpaka mkaogopa mkanyenyekea, tukakwambieni: Shikeni uwongofu na uwongozi tulio kupeni kwa nguvu na jitihadi, na mkumbuke kwa kutekeleza na kutenda yaliyo tajwa ndani ili mpate kujilinda nafsi zenu msipate adhabu.
Tena baada ya hayo yote mkageuka. Na lau kuwa si fadhila na rehema ya Mwenyezi Mungu juu yenu kuiakhirisha adhabu kwenu mngeli kwisha kuwa miongoni walio potea na kuangamia.
Na nyinyi bila ya shaka mliwajua wale walio pindukia mipaka katika siku ya Sabato, siku ya ibada na mapumziko, siku ya Jumaamosi. Pale walipo kwenda kuvua samaki siku hiyo na ilhali siku hiyo ilikuwa imetengwa iwe ni siku ya mapumziko na siku kuu, na kufanya kazi siku hiyo ilikatazwa. Mwenyezi Mungu alizipotoa nyoyo za wakosefu wale, wakawa kama manyani katika pumbao lao na matamanio yao. Tukawaweka mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu, wakifukuzwa kama mijibwa, watu hawataki kukaa nao, na wanawanyanyapaa kuchanganyika nao.
Mwenyezi Mungu ameifanya hali yao namna hii waliyo ifikia ili iwe ni kama funzo na onyo kwa wengineo, wasitende kitendo kama hichi. Ameyafanya haya ili yazingatiwe na watu wa nyakati zao na watakao kuja baada yao, kama tulivyo yafanya kuwa ni mawaidha kwa wale wanao mcha Mola wao Mlezi, kwani wao ndio wanao nafiika kwa maonyo ya mawaidha na mazingatio.
Na kumbukeni pale alipo uliwa mtu na asijuulikane muuwaji, Musa akawaambia watu wake: Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mchinje Ng'ombe ili iwe ndio ufunguo wa kumgundua muuwaji. Lakini wakaona hayo ni mageni, baina ya yale mauwaji na kumchinja ng'ombe. Wakasema: Unatufanyia maskhara wewe Musa? Yeye akawajibu: Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu asinipatilize kwa kuwa katika wajinga wanao wadhihaki waja wake.
Tena wakamwambia Musa wakirejea lile shauri la ng'ombe: Tutakie kwa Mola wako Mlezi atubainishie sifa za huyo ng'ombe. Akawaambia: Mwenyezi Mungu ameniambia huyo Ng'ombe si mkubwa wala si mdogo, bali yu katikati baina ya upevu na uchanga. Basi hebu tekelezeni alivyo kuamrisheni Mwenyezi Mungu
Lakini walikakamia katika kutaradadi kwao, wakasema: Tutakie kwa Mola wako Mlezi atupambanulie nini rangi yake. Akawajibu: Mwenyezi Mungu anasema: Ng'ombe huyo ni wa rangi ya manjano iliyo koza, na safi. Ukimtazama anapendeza kwa usafi wa rangi yake ilivyo zagaa.