Na zipo dalili nyingi na Ishara kwa kila mwenye akili juu ya kuwapo kwake na Ungu wake. Miongoni mwa hizo ni hizi mbingu mzionazo zinazo pitiwa na sayari kwa nidhamu bila ya kuzahamiana wala kugongana, zikiuletea ulimwengu huu joto na nuru. Na pia hii dunia yenye bara na bahari, na kupishana usiku na mchana, pamoja na manufaa yake. Katika Ishara na dalili hizo ni kuzingatia marikebu zipitazo baharini zikibeba watu na vifao vyao, na hapana aziendeshao hizo ila Mwenyezi Mungu. Ni Yeye ndiye anaye zituma pepo zinazo leta mvua. Na mvua ikateremka ikahuisha wanyama na ikanywesha ardhi na mimea. Na hizo pepo kwa mivumo yake ya kila namna, na mawingu yaliyo tundikwa baina ya mbingu na ardhi: Jee, yote haya yamesimama kwa uangalifu namna hii na kwa hukumu kama hizi wenyewe tu? Au vimeundwa na Mwenye Kujua Mwenye Uwezo?
Na juu ya dalili zilio wazi baadhi ya watu walio potelewa na akili wamewafanya miungu mingine isiyo kuwa Mwenyezi Mungu, wakiwat'ii na kuwaabudu kama Mwenyezi Mungu na wakawafanya mfano wa Mwenyezi Mungu. Muumini humuelekea Mwenyezi Mungu tu, na kumt'ii kwake hakuna ukomo. Ama hao ut'iifu wao kwa miungu yao hulegalega wakati wa shida. Hapo basi humkimbilia Allah Subhanahu. Na walio jidhulumu nafsi zao lau wangezingatia adhabu itakayo wapata Siku ya Malipo, utakapo dhihiri Ufalme wa Mwenyezi Mungu, na ut'iifu ukawa wake tu wangeli achilia mbali ukhalifu wao na wangeli sita kutenda dhambi zao.
Siku hiyo wafuasi watatamani wakubwa wao wawaokoe na upotofu, nao watawakataa na kujitenga nao wakisema: Hatukukwiteni mtut'ii katika kumuasi Mola wenu Mlezi. Hilo ni pumbao lenu tu na uovu wa vitendo vyenu. Makhusiano baina yao na mapenzi waliyo kuwa nayo duniani yatakatika siku hiyo, na watakuwa maadui wao kwa wao.
Na hapa wafuasi itawabainikia kuwa walipotea walipo wafuata viongozi wao katika upotovu, na watatamani warejee duniani wawakatae viongozi wao kama wao walivyo wakataa siku ya leo. Vitendo vyao viovu vitadhihiri wajute, lakini wapi! Vimekwisha watumbukiza Motoni, na wala hawatatoka humo.
Enyi watu! Kuleni vyakula alivyo kuumbieni Mwenyezi Mungu katika ardhi vilivyo halali, visivyo harimishwa, vilivyo vizuri, vinavyo pendwa na nafsi. Wala msimfuate Shetani anaye kupendezeni kula chakula cha haramu, au kuharimisha kilicho halali. Nyinyi mmeujua uadui wa Shetani kwenu, na umebainika ubaya wa anayo kuamrisheni.
Shetani anakupambieni kiovu kwa dhati na chenye madhara kwa afya yenu, na kibaya ili mkitende. Kwa sababu yake mnafuata dhana na mawazo yasio na msingi. Mkamsingizia Mwenyezi Mungu kuhalalisha na kuharimisha bila ya dalili ya ilimu na yakini.