Na mtajeni Mwenyezi Mungu kwa Takbiri na vinginevyo katika siku maalumu, nazo ni siku za kutupa mawe hapo Mina, nazo ni taarikh 11 na 12 na 13. Na si lazima kwa Haji kukaa siku tatu hizi Mina akitupa mawe, bali anaweza kufupiza siku mbili, kwani msimamo wa kheri ni kuchamngu, si idadi. Na daima mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kuwa kwake Yeye mtakusanywa na muulizwe mliyo yatenda. Hayo mawe ni changarawe hutupwa mwahala maalumu katika Mina katika siku ya kuchinja (Idd) na siku tatu zifwatiazo.
Ilivyo kuwa kumcha Mwenyezi Mungu ndio msingi, basi khasara ni ya wale watu ambao dhamiri walio nayo nyoyoni mwao ni mbali na maneno yanayo tamkwa na ndimi zao. Wamepewa utamu wa kupanga maneno, hukufurahisha kauli yao katika kujivutia manufaa ya maisha ya kidunia, na kuunga mkono kwa wayasemayo humsingizia Mwenyezi Mungu kuwa anashuhudia kuwa wayasemayo yanatoka nyoyoni mwao. Kumbe wao kwa hakika ndio wakubwa wa ukhasama na ukhabithi kwako wewe.
Na pindi wakitawalishwa madaraka yoyote haiwi juhudi yao kuleta maslaha, bali ni kuleta ufisadi na kuteketeza mimea, kukata miti na kuuwa wanyama na binaadamu. Na Mwenyezi hawapendi watu kama hawa, kwani Mwenyezi Mtukufu hapendi uharibifu.
Akinasihiwa amwogope Mwenyezi Mungu huzidi kupanda mori wake na akadhani kuwa hivyo unamvunjia cheo chake, akazidi kupanda madhambi na kuzidi kumchafua na kumwongeza inadi. Mtu huyo hatoshelezeki mpaka aingie Jahannam, na hayo ni makao maovu mno.
Ni farka kubwa baina ya wanaafiki hawa na Waumini wa kweli ambao watayari kuuza nafsi zao kwa sababu ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kulitukuza Neno la Haki. Hawa ni kinyume na wale wa kwanza. Hawa wakitawalishwa madaraka kuendesha mambo ya watu inakuwa ni katika upole wa Mwenyezi Mungu kuwafanyia waja wake. Mwenyezi Mungu Mtukufu huwarehemu hao waja wema kwa kuwatawalisha watu wema ili awalinde na wenye shari.
Enyi mlio amini! Na iwe baina yenu nyote amani na salama,wala msichochee chuki za kijahiliya na mengineyo kuleta sababu za ugomvi na khitilafu. Wala msipite katika njia ya Shetani anaye kupelekeeni kugawanyika, kwani yeye ni adui wenu aliye dhaahiri. Maneno haya ya Qur'ani ni wito kwa Waumini wote iwe baina yao salama na amani, na yanafahamisha kuwa vita na khasama ni katika mwendo wa kumfuata Shetani. Waumini wote wanaitwa wawe katika hali ya salama na wengineo, na wao baina yao kwa wao, wasipigane na wengine wala wasipigane wenyewe kwa wenyewe. Na maneno haya ya Qur'ani yanaonyesha kuwa mahusiano baina ya dola ya Kiislamu na nyenginezo ni salama, na huo ni msingi wa mwanzo wa dini zote za mbinguni. Wakati ilipo kuwa kanuni ya porini ndiyo inayo hukumu baina ya madola na kuwekea mipaka ya mahusiano yao, mwenye nguvu kumla mnyonge, Uislamu ulikuja na huu msingi wa kuamrisha kuwa mahusiano yawe ya Usalama. Pindi vikitokea vita basi viwe kwa ajili ya ulinzi na kuupinga uvamizi. Yaani ni kumlazimisha yule mwenye kufanya uadui awe mwenye usalama. Vita vilivyo ruhusiwa na Uislamu ni kuthibitisha nguzo za amani, na kuhakikisha uadilifu. Vita hivi ni vita vya salama, kwa ajili ya uadilifu na amani.
Mkigeuka mkaiacha Njia hii mliyo itiwa muifuate nyote baada ya kudhihiri hoja za kukata kuwa ndiyo Njia ya Haki, basi jueni mtapatilizwa kwa kugeuka huko, kwani Mwenyezi Mungu hakika ni Mwenye nguvu, humuadhibu mwenye kuiacha Njia yake, na Mwenye hikima anaye pima kadiri ya adhabu yake.
Je, hao wanao ukataa Uislamu wanangojea mpaka wamwone Mwenyezi Mungu Mtukufu na Malaika jahara katika mawingu na hukumu ya kuwakatisha tamaa zao imekwisha pitishwa? Kwani hakika mambo yote yamo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Yeye huyasarifu atakavyo, na hukumu yake imekwisha tolewa, na hapana shaka yoyote itatekelezwa tu.