Kitaje pia kisa cha Ibrahim alipo sema: Mola wangu Mlezi nionyeshe vipi unahuisha maiti. Mola wake Mlezi akamuuliza Ibrahim, juu ya imani yake kuamini kufufuliwa wafu, ili ajibu Ibrahim kuondoa shaka kabisa katika imani yake. Mwenyezi Mungu akamwambia: Kwani huamini kufufuliwa wafu? Ibrahim akajibu: Mimi naamini, lakini nimetaka ili moyo uzidi kutua. Akasema Mwenyezi Mungu: Basi wachukue ndege wane uwe nao ili uwajue vilivyo. Kisha uwagawe baada ya kuwachinja, na juu ya kila kilima katika vilima vilio jirani weka sehemu yao. Kisha uwete, watakujia mbio, nao ni wahai kama walivyo kuwa. Na jua kuwa Mwenyezi Mungu hashindwi na lolote. Naye ni Mwenye hikima iliyo pita hadi katika kila kitu. Ametaja Al Fakhri Al Razi na wengineo kuwa yapo maoni mengine juu ya tafsiri ya maneno haya matukufu. Nayo ni kuwa Ibrahim hakuwachinja wale ndege, wala hakuamrishwa kuwachinja. Bali aliamrishwa awakusanye kwa kuwazoesha kukaa naye. Kisha akawagawa akaweka juu ya kila kilima ndege mmoja. Kisha akawaita wakamjia. Na hii ni namna Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyo umba, ni kwa amri yake ya "Kuwa" basi huwa, kama alivyo waita wakaja
Hakika hali ya wale wanao toa mali yao kwa ajili ya kumt'ii Mwenyezi Mungu na kufanya kheri, na wanapata kwa hivyo thawabu za kuzidia mara nyingi, ni kama hali ya mwenye kuatika punje moja katika ardhi yenye rutuba ikamea mmea wenye mashuke saba, katika kila shuke mna punje mia. Hii ni sura ya wingi wa Mwenyezi Mungu anavyo walipa wanao toa katika dunia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakae. Yeye ni Mwenye wasaa wa fadhila, Mwenye kuwajua wanao stahiki na wasio stahiki.
Hakika wanao toa mali kwa ajili ya wema unao kubaliwa na sharia bila ya kusimbulia au kutafakhari au kumcheleweshea yule anaye fanyiwa hisani, hao wana malipo bora walio ahidiwa kwa Mola wao Mlezi, wala haiwapati khofu kwa lolote wala huzuni.
Kauli ya kupoza nyoyo na ya kumsitiri hali fakiri usimwambie mwenginewe ni bora kuliko kumpa na baadae ukafuatizia maudhi kwa maneno au vitendo. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la si mwenye kuhitaji watu watoe na huku wanawaudhi mafakiri. Na Yeye anawawezesha mafakiri kupata riziki njema. Wala hafanyi haraka kumuadhibu asiye toa kwa matarajio huenda akaongoka akatoa.
Enyi Waumini! Msipoteze thawabu za sadaka zenu kwa kudhihirisha kuwa mnawafadhili wenye haja na kuwaudhi. Hivyo mnakuwa kama wale wanao toa mali zao kwa ajili ya kutafuta umaarufu na kupenda wasifiwe na watu., nao hata hawamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Hali ya mwenye kuonyesha kutoa kwake ni hali ya jiwe manga lenye udongo. Likateremkiwa na mvua kubwa, udongo wote ukaondoka. Basi kama mvua kubwa inavyo chukua udongo wenye mbolea likabaki jiwe tupu, basi kadhaalika masimbulizi, na maudhi, na kuonyesha watu huharibu thawabu za sadaka. Hayo hayamnufaishi mtu, na hizo ni sifa za makafiri. Epukaneni nazo! Kwani Mwenyezi Mungu hawawafikishi makafiri kupata kheri na uwongozi mwema.