Hali ya watu hawa katika unaafiki wao ni kama hali ya mwenye kuwasha moto apate nafuu yeye na watu wake. Moto ukisha waka ukatoa mwangaza kunawiri kote, Mwenyezi Mungu huwaondolea Nuru wenye kuwasha wakawa katika giza zito, hawaoni chochote. Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwatunukia sababu za kuongoka, nao hawakuzishika. Kwa hivyo macho yao yakazibwa, wakastahiki kubaki katika kuemewa na upotovu.
Watu hawa ni kama viziwi, kwani wamepoteza manufaa ya kusikia; hawaisikii Haki kwa msikio wa kuikubali na kuitikia. Nao ni kama bubu, kwa sababu hawatamki la uwongofu au la Haki. Na wao kama vipofu, kwani hawanufaiki kwa macho yao. Hawazingatii na kujikataza. Basi hao hawaachi upotovu wao.
Au mfano wa hali yao katika kubabaika kwao, na hadi ya mambo yanavyo waemea, na kutokufahamu nini liwafaalo na nini linalo wadhuru, ni kama hali ya watu walio teremkiwa na mvua kutoka mbinguni, yenye radi na mingurumo, wanatia ncha za vidole vyao masikioni mwao ili ati wasisikie sauti za mingurumo, na huku wanaogopa kufa, wakidhani kuwa kule kujiziba kwa vidole kutawalinda na mauti. Watu hao ikiteremka Qur'ani - na ndani yake ikabainisha giza la ukafiri na ikatoa maonyo ya juu yake, na ikabainisha Imani na mwangaza wake unao meremeta, na yakabainishwa mahadharisho na namna mbali mbali za adhabu - wao hujitenga nayo na wakajaribu kuepukana nayo kwa kudai kuwa ati kwa kujitenga nayo wataepukana na adhabu. Lakini Mwenyezi Mungu amewazunguka makafiri kila upande kwa ujuzi wake na uwezo wake.
Huu umeme mkali wa kuonya unakaribia kunyakua macho yao kwa ukali wake, nao kwa hakika unawamurikia njia kidogo ili wapate kwenda khatua chache kwa mwangaza wake, na unapo katika umeme kiza kinazidi, basi wao husimama hawajui watendeje, wamepotea. Basi hawa wanaafiki dalili na ishara zinapo watolea mwangaza huwa na hamu ya kutaka kuongoka, lakini mara punde hurejea kule kule kwenye ukafiri na unaafiki. Mwenyezi Mungu, Mkunjufu wa uwezo akitaka kitu hukitenda tu, haemewi na chochote katika ardhi wala katika mbingu.
Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliye kuanzeni, akakuumbeni akakuleeni, kama alivyo waumba walio kutangulieni. Kwani Yeye ndiye Muumba wa kila kitu. Haya ni hivyo ili mpate kuzitayarisha nafsi zenu, na mzitengeneze kwa ajili ya utukufu wa Mwenyezi Mungu na uangalizi wake. Kwa hivyo nafsi zenu zitahirike na zipate kuifuata Haki, na ziogope mwisho muovu.
Ni Yeye Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye itandika ardhi kwa kudra yake, na akaikunjua ili isahilike kwenu kuweza kuikalia na kunafiika kwayo. Akajaalia juu yenu mbingu zilio nyanyuka na sayari zake mfano wa jengo lililo jengwa vilivyo, na akakuleteeni njia za uhai na neema - nayo ni maji - aliyo yateremsha kutoka mbinguni, akayafanya ndiyo sababu ya kutoa mimea na miti ya matunda ambayo amekuruzukuni faida yake. Basi haifai baada ya haya mkawaza kuwa Mwenyezi Mungu ana washirika mkawaabudu kama kumuabudu Yeye, kwani Yeye hana mfano wake wala mshirika. Na nyinyi kwa maumbile yenu mnajua kwa yakini kuwa Yeye hana mfano wala mshirika. Basi msiyaharibu maumbile haya. Katika Aya hii ipo sehemu ya kuonesha muujiza wa Qur'ani Tukufu: nayo ni kauli yake Mtukufu "mbingu kama paa". Haya asingeyajua Nabii asiyejua kusoma ila kwa ufunuo wa Mwenyezi Mungu, nayo ni kuwa mbingu kwa kisayansi ni kila kilicho izunguka dunia pande zote, na kwa ukomo wowote, na kwa sura yoyote katika anga, mpaka huko juu kabisa kwenye sayari nyenginezo, zilizoenea zisio na mwisho. Zote hizo zinazunguka kwa mpango wa ajabu, na sisi tunapata uvukuto na mn'gao wake, nazo zinakwenda kwa nguvu ya mvutano kama smaku. Katika sehemu ya mwanzo ya mbingu iliyo tuzunguka lipo anga linalo tukinga kama paa na mianga inayo dhuru kutokana na hizo sayari. Na tabaka hizo huachilia mianga yenye faida tu, ndipo penye mawingu yaletayo mvua.
Na ikiwa mna shaka kuisadiki hii Qur'ani tunayo mteremshia mja wetu Muhammad, basi mnayo hoja iliyo dhaahiri itayo kubainishieni haki: jaribuni kuleta sura kama hizi za Qur'ani katika ufasihi wake, na hukumu zake, na ilimu zake, na uwongofu wake wote, na muwaite watakao shuhudia kwamba mmeleta sura mfano wake, mtake msaada kwao, na wala hamtowapata. Na mashahidi hao ni mbali na Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu anamuunga mkono mja wake kwa hichi Kitabu chake, na anamshuhudia kwa vitendo vyake. Haya ikiwa ni kweli nyinyi mnaitilia shaka hii Qur'ani.
Basi ikiwa hamtoweza kuleta sura moja mfano wa hizi sura za Qur'ani - na kabisa hamtoweza kwa njia yoyote, kwani viumbe hawawezi hayo kwa kuwa Qura'ani ni maneno ya Muumba - basi waajibu wenu mziepuke sababu zitazo kuleteeni adhabu ya akhera, nayo ni Moto ambao utakuwa kuni zake za kuwashia ni hao makafiri na masanamu yao. Moto huu umetengenezwa kwa ajili ya kuwaadhibu wapinzani wenye inda.