Ikiwa mko safarini na hamkupata mtu wa kuliandika deni, basi kwa dhamana ya deni wekeni kitu kuwa ni rahani ashike mwenye kukopesha kutokana na mwenye kukopa. Na mtu akipewa dhamana na mwenzie kushika, basi iwe hiyo ni amana ilioko mikononi mwake. Yeye ametegemewa kwa uaminifu wake. Basi inapo takikana amana na aitoe amana ya watu. Na amche Mwenyezi Mungu aliye muumba na kumlea na kumshughulikia kwa uangalifu ili isimkatikie neema ya Mola wake Mlezi duniani na Akhera. Wala msifiche ushahidi unapo takikana. Mwenye kuficha amepata dhambi, na khabithi wa moyo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua mnayo yafanya. Atakulipeni kwa mujibu mnavyo stahiki.
Jueni kuwa vyote viliomo mbinguni na duniani ni vya Mwenyezi Mungu, naye ana makdara navyo vyote na anavijua vyote. Ni sawa sawa ikiwa mtadhihirisha yaliyomo ndani ya nafsi zenu au mkificha, Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa vyote na mwenye kupata khabari za vyote. Naye Siku ya Kiyama atakuhisabuni kwa hayo, na atamghufiria amtakaye na atamuadhibu amtakaye. Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Hakika aliyo teremshiwa Mtume Muhammad s.a.w. ni Haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Naye amemuamini Mwenyezi Mungu, na pamoja naye wameamini pia Waumini, wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake. Wao wanawaamini Mitume wote wa Mwenyezi Mungu sawa sawa, na wanawatukuza sawa, huku wakisema: Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume wake. Na wametilia mkazo Imani yao ya moyoni kwa kauli yao ya ulimini huku wakimuelekea Mwenyezi Mungu kumwambia: Mola Mlezi wetu! Tumesikia uliyo yateremsha yenye hikima, na tumeyapokea yaliyo amrishwa. Ewe Mola wetu Mlezi! Tupe maghfira yako. Na kwako Wewe tu pekee ndio tunako kwendea na ndio marejeo.
Hakika Mwenyezi Mungu hawakalifishi waja wake ila kwa kadiri wanavyo weza kuyafanya na kuyafuata. Kwa hivyo kila mwenye kukalifishwa atalipwa kwa vitendo vyake - akitenda kheri atapata malipo ya kheri, akitenda shari atapata shari. Basi enyi Waumini! Nyenyekeeni kwa Mwenyezi Mungu mkimuomba: Ewe Mola Mlezi wetu! Usituadhibu pindi tukiporonyoka tukasahau ulio tuamrisha, au yakatupata ya kutusabibisha kutumbukia makosani. Mola Mlezi wetu! Usituchukulie kwa shida ukatupa sharia nzito nzito kama ulivyo wafanyia Mayahudi kwa sababu ya inda yao na udhalimu wao. Wala usitukalifishe mambo tusiyo yaweza, na utusamehe kwa ukarimu wako, na tughufirie kwa fadhila yako, na uturehemu kwa rehema yako yenye wasaa. Hakika Wewe ni Mola Mlezi wetu. Tunusuru ewe Mola Mlezi, kwa ajili ya kutukuza Neno lako na kuitangaza Dini yako - tuwashinde kaumu ya wapingaji.