Yule bibi alipo yasikia masengenyo yao wale wanawake na kuwa wanamsema kwa vibaya, aliwaalika nyumbani kwake na akawapangia matakia na mito ya kuegemea, na akampa kila mmoja wao kisu, baada ya kwisha hudhuria na wakakaa wakiegemea. Akawaletea chakula na visu vya kulia. Akamwambia Yusuf: Hebu watokee! Alipotokeza wakamwona walistaajabu. Uzuri wake ulio pita mpaka uliwatwaa wasijitambue, wakawa wanajikata mikono yao jinsi ya kushtuka kwao, na huku wanadhani wanakata chakula! Wakasema kwa mastaajabu na kushituka: Hasha Lillahi! Mungu apishe mbali! Huyu tunaye mwona si binaadamu! Hapana binaadamu mwenye uzuri namna hii, na mwenye jamali kama hivi, na usafi kama huu, na kunyooka kama huku! Huyu ni Malaika tu, mwenye uzuri huu, na sifa hizi zilio timia!
Tena mke wa Mheshimiwa alisema kufuatiliza maneno yao: Huyu kijana ambaye uzuri wake umekuzugeni na ukakuemeeni hata yakatokea yaliyo tokea ndiye ambaye nyinyi mliye nilaumu kwa ajili yake! Na mimi kweli nilimtaka, na nikafanya juhudi kumghuri anikubalie, naye akajizuia na akakataa. Kama kwamba vile anavyo kataa ndio anazidi kumtia hamu yule mwanamke! Akasema mwanamke: Na mimi naapa! Kama hafanyi ninayo muamrisha atapata adhabu ya kifungo, na atakuwa katika madhalili wenye kudharauliwa!
Yusuf akasema naye alisikia vile vitishio, na akasikia kwa wale wanawake nasiha ya kuwa amkubalie, akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nakhiari kifungo kuliko hayo anayo nitakia huyu mwanamke. Kwani hayo ni kukuasi Wewe. Na kama Wewe hunikingi na shari ya vitimbi vyao na hila zao nitakuja wakubalia, na nitakuwa miongoni mwa wajinga walio potea.
Mwenyezi Mungu akamuitikia, na akamuepusha na shari ya vitimbi vyao. Hakika Yeye peke yake ndiye Mwenye kusikia maombi ya wenye kukimbilia kwake, na Mwenye kujua yanao wafaa.
Kisha ikadhihiri rai ya Mheshimiwa na watu wake, baada ya kwisha ona dalili zilizo wazi kuwa Yusuf hana makosa. Wakakubaliana rai hii, na wakaapa kuitimiza. Nayo ni kumtia yeye gerezani kwa muda mfupi au mrefu, ili kumkinga mkewe na maneno mabaya, na kumuepusha na masengenyo ya watu!
Wakaingia pamoja na Yusuf vijana wawili katika watumishi wa Mfalme. Mmoja wao akasema: Mimi nimeota usingizini kuwa ninakamua zabibu kutengeneza mvinyo. Mwingine akasema: Mimi nimeota nimebeba kichwani mwangu mikate, na ndege wanaila! Hebu tuambie, ewe Yusuf, tafsiri ya haya tuliyo ota, na mambo yetu yataishia vipi. Sisi tunaamini kuwa wewe ni katika watu wanao sifika kwa wema na kujua tafsiri za ndoto.
Yusuf akawaambia kutilia mkazo yale waliyo yajua kwake Yusuf: Hakitowahi kukufikieni chakula kuwa ni riziki mliyo kadiriwa ila nami nitakwambieni kitavyo kujieni kabla ya kukufikieni. Na nitakutajieni mapishi yake na vipi kilivyo. Namna hivyo ndivyo tafsiri ya ndoto na khabari zilizo fichikana katika alivyo nifunza Mola wangu Mlezi na akanifunulia, kwani nilimtakasia Yeye tu ibada yangu. Na nikakataa kumshirikisha na kitu chochote. Na nikajitenga mbali na dini ya watu wasio msadiki Mwenyezi Mungu, na wala hawamuamini Yeye kwa njia iliyo sawa, nao wanaikanya Akhera na hisabu zake.