Akashikilia tamaa yake akingojea rehema ya Mwenyezi Mungu, na ahali zake wakashikilia kumdhania dhana mbovu mpaka alipo fika mtu aliye chukua kanzu na kumbashiria kwamba Yusuf yupo salama salmina. Ilipo wekwa kanzu usoni kwa Yaa'qub akainusa harufu yake, moyo wake ulijaa furaha, macho yake yakarejea kuona. Yule mjumbe alipo msimulia hali ya Yusuf, na kwamba anamtaka yeye asafiri ende pamoja na ahali zake, aliwageukia walio kuwa naye akiwakumbusha ule utabiri wake, na akiwakaripia kwa vile walivyo mkadhibisha. Akawataka wakumbuke yale aliyo wahakikishia pale punde kwamba yeye anaijua rehema ya Mwenyezi Mungu na fadhila yake wasio ijua wao.
Hapo wakamkabili kwa kumtaka msamaha, wakimtaraji awasamehe, na awatakie kwa Mwenyezi Mungu maghfira kwa madhambi yao. Kwani wao walimhakikishia katika kule kutubu kwao kwamba wao walikuwa ni wenye kutenda madhambi.
Akasema Yaa'qub nitaendelea kutaka msamaha kwa Mwenyezi Mungu kufutiwa dhambi zenu. Na hakika Yeye peke yake ndiye mwenye maghfira ya milele na rehema ya daima.
Yaa'qub akasafiri kwenda Misri pamoja na ahali zake mpaka akafika huko. Walipo ingia kwa Yusuf, naye alikuwa kawapokea kwenye milango ya Misr, huruma na shauku ilimpeleka kwa haraka kwa baba na mama yake! Akawakaribisha na akawataka wao na ahali zake wakae Misri kwa amani na salama kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Msafara ukenda ndani ya nchi ya Misri mpaka ukafika kwenye nyumba ya Yusuf. Wakaingia, na Yusuf akawatanguliza wazazi wake akawaweka kwenye kochi. Yaa'qub na ahali zake wakajaa furaha kwa uzuri wa mapokezi aliyo watengezea Mwenyezi Mungu katika mikono ya Yusuf. Kwani kwa hayo ukoo wote umekusanyika hapo baada ya mfarakano, na umetukuka makamu makubwa ya utukufu na hishima. Wakamuamkia maamkio yaliyo zowewa na watu tangu zamani ya kuwaamkia maraisi na watawala. Wakaonyesha unyenyekevu kwa utawala wake. Yale yalimkumbusha Yusuf ile ndoto yake ya utotoni. Akamwambia baba yake: Hii ndio tafsiri ya ndoto niliyo iota na nikakusimulia ya kwamba nimeota usingizini kuwa nyota kumi na moja na jua na mwezi zinanisujudia; ni hivi basi Mola wangu Mlezi ameitimiza, na amenitukuza na amenifanyia hisani. Amedhihirisha kuwa sina makosa, na akanitoa kifungoni, na akakuleteni kutoka jangwani tukutane, baada ya Shetani kutufisidi baina yangu na ndugu zangu, akawachochea dhidi yangu. Na haya yote yasinge kuwa bila ya Mwenyezi Mungu kuyafanya. Yeye ndiye wa kupanga na kuyafanya mambo yatimie kama atakavyo. Na Yeye ndiye Mwenye kuzunguka kila kitu kwa ujuzi wake, ambaye hukumu yake ni yenye kushinda katika kila jambo na kadhiya.
Yusuf akamwelekea Mwenyezi Mungu akimshukuru kwa kuzihisabu neema zake juu yake, na akimwomba amzidishie fadhila zake, kwa kusema: Ewe Mola wangu Mlezi! Neema zako kwangu ni nyingi mno, na bora mno! Umenipa utawala, na nakuhimidi kwa hayo. Ukanitunukia ilimu ya kufasiri ndoto kama ulivyo nitunukia! Ewe Muumba mbingu na ardhi! Wewe ndiye uliye miliki mambo yangu yote, na Mtawala wa neema za uhai wangu na baada ya kufa kwangu! Nifungamanishe nawe kwa ulivyo waridhia Manabii wako katika Dini ya Kiislamu, na uniingize katika kundi la ulio waongoa kwenye wema miongoni mwa baba zangu, na waja wako walio wema, walio safika.
Ewe Nabii! Haya tuliyo kusimulia ni katika khabari zilizo pita za kale. Hazikukufikia ila kwa wahyi ulio toka kwetu. Wala wewe hukuwapo pale nduguze Yusuf walipo kuwa wakipanga njama. Wala wewe hukuwa unavijua vitimbi vyao ila kwa kusimuliwa nasi.
Na wapo wengi ambao tabia zao zina maradhi zinazo wazuia wasisadiki haya unayo funuliwa, hata moyo wako ukiwa una shauku namna gani waamini, au nafsi yako ikafanya juhudi gani waongoke.