Basi baada ya kuwakirimu kwa kuja kwao, na kuwapimia chakula, na kuwazidishia shehena ya nduguye, aliwafungia mizigo yao kwa ajili ya safari. Tena akawaamrisha wasaidizi wake watumbukize chombo cha kunywea katika mzigo wa Bin-yamini. Kisha mmoja wa wasaidizi wa Yusuf alinadi: Enyi wasafiri! Ngojeni! Nyinyi ni wezi!
Wale wasaidizi wakajibu: Tunatafuta kikopo, nacho ni chombo anacho nywea mwenyewe mfalme. Na malipo yake kwa mwenye kukileta ni shehena nzima ya chakula anayo ibeba ngamia. Yule mkubwa wao alitilia mkazo hayo kwa kusema: Na mimi ninadhamini kutimiza ahadi hii.
Nduguze Yusuf wakasema: Hakika kututuhumu sisi kwa wizi ni jambo la ajabu mno! Na tunahakikisha kwa kiapo ya kwamba nyinyi wenyewe mmeona katika mwendo wetu na tunavyo ishika dini yetu katika mara mbili tulipo kuja hapa kuwa mmejua yakini kuwa sisi hatutaki kuleta uharibifu katika nchi yenu. Wala si katika tabia yetu kuwa ni wezi.
Na Yusuf alikwisha waamrisha wafwasi wake wawaache nduguze waamue nini malipo anayo stahiki kupata yule atakaye onekana nacho kile kikopo, ili apate kumchukua nduguye kwa hukumu yao wenyewe, na iwe hukumu yao ndiyo ya kukata shauri, isiwepo njia ya kumwombea. Basi watu wa Yusuf wakawaambia wale nduguze: Nini malipo ya wevi kwenu wanapo gundulikana ni katika nyinyi?
Na kwa kuwa wana wa Yaa'qub walikuwa na yakini kuwa wao hawakukiba kile kikopo walisema bila ya kusitasita: Malipo ya mwenye kuchukua hicho kikopo ni kushikwa huyo na afanywe mtumwa. Ndio hivi sisi tunavyo walipa wenye kudhulumu wakachukua mali ya watu.
Shauri ikaishia ipekuliwe mizigo, na ikawa lazima kufanya mambo baraabara ili isionekane kuwa kuna mpango ulio pangwa. Yusuf mwenyewe ndiye aliye fanya uchunguzi, baada ya kwisha tengeza mambo. Akaanza kupekua mizigo ya wale ndugu kumi, kisha ndio akaingia kuupekua mzigo wa nduguye. Humo akakitoa kile kikopo, na kwa hivyo hila yake ikafuzu. Akawa na haki kwa hukumu ya nduguze kumshika Bin-yamini. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu alivyo mpangia mambo Yusuf. Hakuwa anaweza yeye kumshika nduguye kwa mujibu wa sharia ya mfalme wa Misri tu ila kwa kutaka Mwenyezi Mungu. Naye alitaka. Basi tulimpangia mambo Yusuf, na tukamwezesha kuzirekibisha sababu na mipango baraabara na hila nzuri. Na haya ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu, ambaye humtukuza katika vyeo vya ujuzi amtakaye. Na juu ya kila mwenye ilimu yupo mwenye kumzidia katika ujuzi!
Kule kugunduliwa kikopo katika mzigo wa ndugu yake kwa ghafla kuliwashangaza nduguze na kukawababaisha. Kwa hivyo wakataka kujivua kuwa wao wote hawana makosa ila huyo na Yusuf, na kusema kuwa tabia ya wizi wameirithi kwa mama yao. Wakasema: Si ajabu kuwa huyo kaiba, kwani nduguye khalisa aliwahi kwiba vile vile! Na Yusuf akatambua kijembe chao wanacho mpigia, na yakamuudhi hayo. Lakini aliyaficha, na akawawekea jawabu moyoni mwake lau kuwa amesema wazi jawabu yenyewe inge kuwa hivi: Nyinyi mko katika hali ovu zaidi, na nyinyi ni duni zaidi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema, na kutambua ukweli wa maneno yenu ya kumsingizia nduguye fedheha ya wizi.
Wakawa hawana budi kujaribu kumvua ndugu yao au kumtolea fidia kwa kutaka kutimiza ile ahadi yao waliyo mpa Yaa'qub. Wakaingia kutaka kumlainisha moyo Yusuf kwa kumtajia uzee wa baba yao, wakamwambia: Ewe Mheshimiwa! Huyu ndugu yetu ana baba mtu mzima sana. Basi mfanyie huruma umchukue mmoja wetu mwenginewe awe badala ya mwanawe huyu ambaye ndiye anaye mpenda moyoni mwake. Matarajio yetu ni kuwa utatukubalia mambo yetu. Kwenu tumekwisha ona tabia yako ya ukarimu, na tumehakikisha mwendo wako wa kupenda kufanya hisani na kutenda mema.