Na yule bibi aliye kuwa Yusuf anakaa nyumbani kwake, naye anamjua madaraka yake, alitaka kumghuri aache mwendo wake ulio safi. Akawa anajipitisha pitisha mbele yake kuonyesha uzuri wake, na kujitamanisha kwake. Hata mwishoe akamfungia milango, na akamwambia: Njoo kwangu, nimejitoa kwako! Yusuf akasema: Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu, aniepusha na hiyo shari! Na vipi nifanye uchafu huo nawe, na mumeo mheshimiwa ni bwana wangu aliye niweka bora ya makamo? Hakika hawafuzu wanao wadhulumu watu kwa udanganyifu na khiana, wakajitia wenyewe katika maasi ya uzinzi!
Na yule bibi aliazimia aingiane naye, na nafsi ya Yusuf ilimvutia kwake, lau kuwa hakuiona nuru ya Mwenyezi Mungu ya haki imezagaa mbele ya macho yake. Basi hakuufuata mvutio wa nafsi, na akayashinda matamanio, na akajizuilia maasi na khiana. Akathibiti juu ya usafi na kutakasika kwake. Ndio hivi tulivyo mthibitisha Yusuf kwenye usafi na kutakasika, ili tumuepushe na uovu wa khiana na maasi ya uzinzi. Hakika yeye ni miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu walio itakasa dini yao kwa Mwenyezi Mungu.
Yusuf akakimbilia mlangoni kutaka kutoka, na yule bibi naye akapiga mbio amtangulie ili amzuie kutoka. Akaivuta kanzu yake kwa nyuma ili kumzuia, akaichana. Hapo wakapambana na mume wa yule bibi mlangoni! Yule bibi akasema kumchongea Yusuf: Hapana malipo ya mwenye kutaka kumfanya mkeo mambo mabaya ila atiwe gerezani, au akutishwe adhabu chungu!
Yusuf akasema kujitetea: Ni yeye ndiye aliyenitaka, na akajaribu kunikhadaa! Ikawa ni kusutana. Alikata hukumu mmojapo katika jamaa zake mwenyewe yule mwanamke kwa kusema: Ikiwa kanzu yake imechanwa mbele, basi huyu bibi kasema kweli katika madai yake, na huyu kijana ni mwongo kwa aliyo yasema.
Na ikiwa kanzu yake imechanwa nyuma, basi huyu mwanamke kasema uwongo, na kijana ni mkweli kwa aliyo yasema.
Mume alipoona kuwa kanzu ya Yusuf imechanwa mgongoni alimwambia mkewe: Huku kumtuhumu kwako kijana kwa yaliyo tokea na hali yeye hana makosa, ni katika vitimbi vyenu, enyi wanawake. Hakika vitimbi vyenu ni vikuu mno!
Ewe Yusuf wachilia mbali mambo haya, na wewe yafiche wala usiyaseme. Na wewe, mwanamke, omba maghfira kwa dhambi yako. Hapana shaka kuwa wewe ni katika wenye dhambi, wenye kuyakusudia makosa, na kutenda maasi, na kuwasingizia wengine uasi wasio ufanya!
Khabari zikawafikia baadhi ya wanawake wa mjini, wakazungumza wakisema: Mke wa Mheshimiwa anamzaini mtumishi wake na anamkhadaa amkubalie anayo yataka kwake! Ama kweli amesalitika kwa mahaba hata hajitambui! Hakika sisi tunaamini kuwa kwa mwendo wake huu ameingia kwenye upotovu na makosa yaliyo wazi.