Na miongoni mwa wanaafiki walikuwapo jamaa walio jenga msikiti si kwa kutafuta ridhaa ya Mwenyezi Mungu, bali wakikusudia madhara, na kufuru, na kuwagawa Waumini. Na wao wataapa kuwa wao hawakutaka kwa kujenga msikiti huo ila kheri na a'mali njema. Na Mwenyezi Mungu anawashuhudia kuwa ni waongo katika hiyo Imani yao. Msikiti ulio tajwa katika Aya ulijengwa na baadhi ya wanaafiki wa Madina walio azimia shari. Waliudhika kujengwa Masjid Qubaa walio ujenga Banu Amri bin Auf, na akaubariki Mtume s.a.w. kwa kuswali ndani yake. Basi Ibn Aamir Arrahib (aliye itwa Rahib, Mmonaki, kwa kushirikiana kwake na Mapadri) aliwachochea hao wanaafiki wajenge nao Msikiti wa ushinde kushindana na walio jenga Masjid Qubaa, ili uwepo ushinde wa kijahili kwa kila mmoja kujitapa kwa kujenga msikiti. Vile vile ilikuwa azma yao wafanye hapo ni kioteo pa kukutania siri kupanga njama za kuwadhuru Waumini. Baada ya kwisha jenga walimualika Mtume s.a.w. ende kuswali humo, wafanye hiyo sala ndio ada tena ya ushindani wao na kuwafarikisha Waumini. Mtume alitaka kuitikia wito wao bila ya kujua njama zao. Lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu alimjuvya alipo kuwa anarudi kutoka vita vya Tabuk na azma yake ya kuitikia wito. Na Yeye Subhanahu akamkataza asisimame kabisa katika msikiti huo, licha ya kuswali ndani yake.
Ewe Mtume! Usisali kabisa katika msikiti huo. Msikiti unao faa kupata rehema za Mwenyezi Mungu na radhi zake tangu mwanzo kama Masjid Qubaa ndio unao stahiki kusimamishwa ndani yake ibada za Mwenyezi Mungu. Katika msikiti huo wamo watu wanao penda kujinadhifisha miili yao na nyoyo zao kwa kutekeleza ibada zilizo sawa. Na Mwenyezi anawapenda na anawalipa thawabu wanao jikaribisha kwake kwa kujit'ahirisha nje na ndani, kiwiliwili na kiroho.
Hawi sawa katika itikadi yake wala katika vitendo vyake mwenye kusimamisha jengo lake kwa usafi wa niya katika kumcha Mwenyezi Mungu na kutafuta radhi zake, na yule mwenye kusimamisha jengo lake juu ya unaafiki, na ukafiri. Kwani vitendo vya mchamngu vimenyooka, vimejengeka juu ya msingi madhbuti. Na vitendo vya mnaafiki ni kama jengo lililo jengwa juu ya ukingo wa shimo. Jengo hilo litaporomoka tu, na litamtupa mwenyewe katika Moto wa Jahannamu. Na Mwenyezi Mungu hamuongoi kwenye Njia ya Uwongofu anaye shikilia kujidhulumu nafsi yake kwa ukafiri.
Na hilo jengo lao walilo lijenga wanaafiki litakuwa ni sababu ya kuwakereketa na kuwatia khofu katika nyoyo zao. Hayeshi hayo mpaka zipasuke nyoyo zao kwa majuto na kutubu au wafe! Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu, na Mwenye hikima katika vitendo vyake na malipo yake.
Mwenyezi Mungu anatilia mkazo ahadi yake aliyo wapa Waumini wanao toa nafsi zao na mali yao kwa ajili ya Njia yake, kuwa hakika Yeye amenunua kwao hizo nafsi zao na mali yao kwa kuwalipa Pepo kuwa ndio thamani ya hivyo walivyo toa. Kwani wao wanapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Wanawauwa maadui wa Mwenyezi Mungu, au wao wanakufa mashahidi katika Njia yake. Na Mwenyezi Mungu amethibitisha ukweli huu katika Taurati na Injili, kama alivyo thibitisha katika Qur'ani. Wala hapana yeyote mwenye kumshinda Mwenyezi Mungu katika kutimiza ahadi. Basi furahini, enyi Waumini Mujaahidina, kwa biashara hii mlio uza nafsi zenu na mali yenu ambayo yatatoweka, na badala yake mkanunua Pepo itakayo baki milele. Na biashara hii ndio ushindi mkubwa kwenu.