Wala usifurahie na moyo wako ukavutika kwa unavyo waona wanaafiki wana mali na wana. Kwani Mwenyezi Mungu hakuwapa hayo ila wapate kuyahangaikia hayo kwa taabu na mashaka wayalinde katika maisha ya duniani, bila ya kupata malipwa yake. Yawakumbe mauti nao wamo katika ukafiri wao, waadhibiwe kwa sababu yake Akhera.
Na hawa wanaafiki hukuapieni kiapo cha uwongo, enyi jamaa Waumini, kwamba wao ni Waumini kama nyinyi. Na hakika wao hawamuamini Mwenyezi Mungu. Lakini hao ni watu madhaifu na woga, na hayo ndiyo yanayo wapelekea kufanya unaafiki wao, na daima kuwa na khofu.
Wao hali wanakudhikini na wanachukia kuingiana nanyi, lau wangeli pata ngome, au mapango milimani, au mashimo chini ya ardhi wakaingia humo, basi wangeli yakimbilia mbio!
Na baadhi ya hawa wanaafiki wanakusema kwa ubaya, na wanakutia ila katika ugawaji wa sadaka na ngawira. Hawana ila uroho wa makombo ya kidunia tu. Ukiwapa wakitakacho wanakuwa radhi nawe kwa utendayo. Na kama hukuwapa ndio wao ni wepesi wa kukuletea maudhi.
Na lau kuwa hao wanaafiki wanao kusema kwa vibaya katika ugawaji wa sadaka na ngawira wangeli ridhia wanacho gaiwa na Mwenyezi Mungu, nacho ndicho anacho wapa Mtume wake, na zikatua nafsi zao - ijapo kuwa ni kitu kidogo - na wakasema: Hukumu ya Mwenyezi Mungu imetutosheleza, na Mwenyezi Mungu ataturuzuku kutokana na fadhila yake, na Mtume wake atakuja tupa zaidi kuliko alicho tupa mara hii, na sisi tunataka ut'iifu wa Mwenyezi Mungu na fadhila zake na ihsani zake.. lau wangeli fanya hayo ingeli kuwa kheri kwao.
Zaka iliyo faridhiwa haitumiwi ila kwa mafakiri wasio pata cha kuwatosha, na masikini wagonjwa ambao hawawezi kazi wala hawana mali, na wale wanao itumikia kwa kuikusanya, na wanao tiwa moyo kwa sababu wanatarajiwa kusilimu na kupatikana kwao manufaa kwa utumishi wao na kuunusuru Uislamu, na wale wanao eneza Uislamu na kufanya tabshiri (Da'awa), na katika kuwakomboa waliomo utumwani na walio tekwa, na kuwatoa waliomo katika unyonge na utawala wa madhila, na katika kuwalipia wenye madeni walio shindwa kuyalipa ikiwa hayo madeni hayakutokana na madhambi au dhulma au upumbavu, na katika kuzatiti Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na katika mambo kama hayo yaliyomo katika njia za kheri na wema, na katika kusaidia wasafiri walio katikiwa kupata msaada wa mali yao na watu wao. Mwenyezi Mungu ameyatungia sharia hayo kuwa ni waajibu kwa ajili ya maslaha ya waja wake. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mwenye kujua vyema maslaha ya viumbe vyake, na Mwenye hikima kwa anayo yafanyia sharia. Zaka ni mpango ulio wekwa wa kukusanya mali kutokana na matajiri na kurudishiwa mafakiri. Kwa hivyo ni haki ya mafakiri katika mali ya matajiri. Na huyakusanya mtawala na huyatumilia kwa njia zake ambazo zinahisabiwa kuwa ndio muhimu kabisa na bora hizo ni kupiga vita athari za ufakiri kwa mafakiri. Hupewa mafakiri, masikini, wasafiri, kusaidiwa mwenye deni aliye kopa kwa jambo la halali si kwa uharibifu, na katika hayo ipo njia ya kupewa mkopo "kardhan hasanan" (mkopo kwa Lillahi). Katika mwanzo wa Uislamu ilivyo kuwa Zaka inatozwa na kutumiwa vilivyo hapakuwapo katika umma mtu anaye lala na njaa, wala mwombaji aliye dhalilika kwa haja. Ilifika hadi hata wenye kutumikia Zaka wakashitaki kuwa jinsi ya kuenea neema hapana wa kustahiki kupewa. Alishitaki mmoja wapo katika Afrika kumshitakia Khalifa Umar bin Abdulaziz kuwa hakumpata fakiri wa kumpa Zaka. Umar akamwambia walipie wenye madeni. Akawalipia. Bado akashitaki tena. Akamwambia wanunue watumwa uwape uhuru wao. Huo basi ndio utumiwaji wa Zaka. Na ukitaka kweli, ni kuwa lau kuwa Zaka zikikusanywa kwa inavyo faa, na zikatumiliwa zinavyo stahiki basi huo bila ya shaka ungeli kuwa ni mpango bora kabisa wa kudhamini maisha ya umma yasipate shida ya umasikini.
Na wapo watu wanaafiki wanakusudia kumuudhi Nabii, na kumletea ya kumkirihi. Wao humtuhumu kuwa anapenda kusikiliza kila analo ambiwa, kweli na uwongo, na kwamba yeye anakhadaika na hayo anayo yasikia. Basi, ewe Mtume! Waambie: Huyo mnaye msengenya nyuma yake sio kama mnavyo dai. Bali yeye ni sikio la kheri kwenu. Hasikii ila la kweli, wala hakhadaiki na upotovu. Anamsadiki Mwenyezi Mungu na wahyi (ufunuo) wake, na anawasadiki Waumini, kwa sababu Imani yao inawakataza uwongo. Na yeye ni rehema kwa kila mmoja wenu anaye amini. Na hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia wanao muudhi Mtume adhabu chungu, na kali, na ya kudumu milele.