Enyi Waumini! Akinadi mwenye kunadi kuwa kuna Jihadi, basi itikieni wito huo, mkiwa mmoja mmoja au kwa makundi. Kila mmoja kwa kadri ya uwezo wake, na hali mna uchangamfu kwa nguvu na salama na silaha. Na muwanie Jihadi kwa mali na nafsi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kulitukuza Neno la Mwenyezi Mungu. Katika hayo upo utukufu na kheri kwenu, ikiwa nyinyi ni watu wenye ujuzi ulio baraabara na mnaijua Haki. Na katika maana yaliyo kusudiwa hapa ni: kuwa nendeni mmepanda au kwa miguu, mna silaha nyepesi na nyengine nzito. Na hivi ni katika mbinu maarufu za kisasa. Silaha nyepesi kama panga ni za kuuwana na askari, na silaha nzito ni za kubomoa ngome za maadui.
Qur'ani inawasusuika wanaafiki kwa kubakia nyuma wakaacha kumfuata Mtume katika Jihadi. Ikasema: Ingeli kuwa walicho itiwa hawa wanaafiki ni pato la kidunia lilio jepesi kulipata, au ingeli kuwa safari yenyewe ya kwendea ni nyepesi, wangeli kufuata, ewe Mtume. Lakini wanaona safari hii ina mashaka! Na watakuapia kwamba lau wangeli weza wangeli toka nawe! Na kwa unaafiki huu na uwongo wanajihilikisha nafsi zao. Na hali haimfichikii Mwenyezi Mungu. Yeye anaujua uwongo wao na atawalipa malipo yake.
Mwenyezi Mungu amekusamehe, ewe Mtume, kwa kuwaruhusu hawa wanaafiki wabaki nyuma wasende kwenye Jihadi kabla ya kuwa haijabainika kwako ukajua kwamba udhuru wao ni wa kweli, na kuwajua walio waongo kati yao katika madai yao kuwa wanaamini, na kuwa ati wana udhuru za kweli..
Sio mwendo wa Waumini wa kweli wanao muamini Mwenyezi Mungu na Hisabu ya Siku ya Mwisho waje kukutaka ruhusa ya kuto kwenda kuwania Jihadi kwa mali na nafsi, au kuwa wao wabaki nyuma wakuache wewe. Kwa sababu ukweli wa Imani yao unawapendekezesha Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua ukweli wa niya za Waumini.
Wanao kutaka ruhusa ni wale wasio muamini Mwenyezi Mungu kwa Imani ya kweli, wala hawaamini Hisabu yake ya Siku ya Mwisho. Kwa sababu nyoyo zao daima zimo katika shaka na wasiwasi. Nao wanaishi katika hali ya ubabaishi. Na watakuja yapata malipo ya hayo.
Na kama kweli hawa wanaafiki walikuwa na niya ya kwenda kwenye Jihadi pamoja na Mtume, wangeli jitayarisha kwa vita na wakajiandalia. Lakini Mwenyezi Mungu Mwenyewe alichukia huko kutoka kwao, kwa kuwa akijua lau wangeli toka nanyi basi wangeli kuwa dhidi yenu si wenzenu. Basi akawatia uzito wasitoke kwa vile nyoyo zao zilivyo jaa unaafiki! Na msemaji wao akasema: Kaeni pamoja na wale wanao kaa wenye udhuru!
Na pindi wangeli toka pamoja nanyi wasinge kuzidishieni nguvu zozote. Lakini wao wangeeneza wasiwasi na kuzidisha fitna, na wakaieneza kati yenu. Na miongoni mwenu wapo wasio jua uovu wa niya zao, na huenda pengine wangeli khadaika na maneno yao, na wakazisikiliza fitna zao. Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema hao wanaafiki, wanao jidhulumu nafsi zao kwa ule uharibifu wanao udhamiria.