Kisha tukawatuma Mitume wetu wakifuatana, kila mmoja kwa kaumu yake. Kila akija Mtume kwa kaumu yake waliukadhibisha wito wake. Nasi tukawateketeza mfululizo, na tukazifanya khabari zao ni hadithi za watu kusimuliana na kuzistaajabia. Basi hao kaumu wasio isadiki Haki wala hawaifuati wametengeka mbali na rehema, na wamehiliki.
Kisha tukamtuma Musa na nduguye, Haaruni, tukawapa dalili za kukata kuthibitisha ukweli wa ujumbe wao, na hoja wazi yenye kudhihirisha kuwa wao ni kweli wametumwa kutoka kwangu.
Tuliwatuma wawili hao kwa Firauni na kaumu yake. Wakakataa kuamini kwa ajili ya takaburi, na wao ni watu walio kuwa wakisifika kwa kiburi, na majivuno, na ujeuri.
Wakasema kwa mastaajabu na kukanya: Je, tuuamini wito wa watu wawili walio ni wanaadamu kama sisi, na tena watu wao hawa Wana wa Israili ni wenye kutunyenyekea sisi na kutut'ii kama ni watumwa?
Na tumemjaalia Isa bin Maryamu na mama yake, kwa vile kuchukua mimba bila ya kuingiliwa na mtu, na kuzaliwa yeye Isa bila ya baba, kuwa dalili ya kukata ya uwezo wetu wenye kushinda. Na tukamweka Maryamu pahala pa kukaa penye ardhi iliyo nyanyuka na kukunjuka panapo faa kukaa, na pana maji mengi. Na hayo ndiyo yanayo wezesha maisha ya starehe.
Tumewaambia Mitume wawafikishie watu wao: Kuleni vyakula vya kila namna vya halali na vizuri, na stareheni na ishukuruni neema yangu kwa vitendo vyema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa myatendayo na nitakulipeni kwayo.
Na tukawaambia wawafikishie watu wao: Hakika hii Dini niliyo kutumeni muifikishe ni Dini moja kwa mintarafu ya Imani na misingi ya sharia. Na hakika nyinyi ni umma mmoja katika vizazi vyote. Miongoni mwao wapo walio ongoka, na wapo walio potoka. Na Mimi ndiye Mola wenu Mlezi niliye kuamrisheni muifuate, basi iogopeni adhabu yangu pindi mkiasi.
Lakini watu walilikata kata hili jambo la Dini yao. Wapo kati yao walio ongoka, na wapo walio potoka ambao wakafuata matamanio yao, wakafarikiana kwa sababu hiyo wakawa makundi mbali mbali yenye kufanyiana uadui. Kila kikundi kinafurahi kwa walio nayo, kwa kudhania kuwa wao tu ndio walio sibu.
Ndio basi Sisi tumekuwa radhi nao, na kheri zikawamiminikia mbio mbio na kwa wingi? Hao ni kama wanyama, hawatambui, kwa kuwa hawazitumii akili zao. Mimi si radhi nao. Na hizi neema ni kuwapururia tu, kuwapa muda.