Na ukisha panda na ukatua wewe na walio pamoja nawe katika jahazi hiyo basi sema kwa kumshukuru Mola wako Mlezi: Alhamdulillahi! Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye ndiye aliye tuokoa na shari ya watu makafiri walio asi.
Na useme: Ewe Mola Mlezi! Nijaalie nishuke mashukio yenye baraka, pahala pazuri pa kukaa wakati wa kuteremka nchi kavu. Na unitunukie amani hapo. Kwani ni Wewe tu peke yako unaye weza kututeremsha pahala pa kheri na amani na salama.
Hakika katika kisa hichi yapo mazingatio na mawaidha mengi. Na hakika Sisi tunawajaribu (tunawapa mitihani) waja wetu kwa kheri na shari. Na ndani ya nafsi zao wana utayarisho wa yote hayo.
Tukawapelekea Huud. Naye ni katika wao. Tukawaambia kwa ulimi wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu peke yake. Kwani nyinyi hamna Mungu anaye stahiki kuabudiwa asiye kuwa Yeye. Ni Yeye peke yake anaye faa mumwogope. Basi, jee mmeikhofu adhabu yake mkimuasi?
Na wakubwa katika kaumu yake walio kufuru na kukadhibisha kukutana na Mwenyezi Mungu na mambo ya Akheria ya hisabu na malipo, na tukawapa sehemu kubwa ya starehe na neema, wakasema kwa kukanusha wito wake, na kuwazuia watu wasimfuate: Hapana khitilafu yo yote baina ya Huud na nyinyi. Anakula chakula hicho hicho mnacho kila nyinyi. Na anakunywa vinywaji hivyo hivyo mnavyo vinywa nyinyi. Mfano wa huyu hawezi kuwa Mtume, kwa sababu hana sifa msizo kuwa nazo nyinyi.
Na wakawahadharisha kwa nguvu na mkazo, wakiwaambia: Mkimt'ii mtu aliye kama nyinyi kwa utu wake, basi nyinyi hakika mtakuwa mmekhasiri kwa kuwa hamtapata manufaa yo yote mkimfuata.
Wakawaambia pia katika kukanya kufufuliwa: Hivyo Huud anakuahidini kuwa mtafufuliwa kutoka makaburini kwenu baada ya kwisha kufa kwenu, na mkawa udongo na mafupa yasiyo kuwa na nyama na mishipa?
Hapana uhai ila mmoja tu. Nao ndio huu uhai wa duniani, ambao tunauona una mauti na uhai unao tupitia. Kinacho zaliwa kinazaliwa, na kilicho hai kinakufa. Wala hatutofufuliwa baada ya kwisha kufa kabisa.
Huyu si chochote ila ni mtu aliye mzulia Mwenyezi Mungu, na akadai kwamba Mwenyezi Mungu kamtuma yeye. Na amesema uwongo katika hayo anayo tuitia. Wala hatutomsadiki abadan. *
Ukawachukua ukelele mkali ulio wahilikisha kama walivyo stahiki. Tukawafanya kwa udhalili na udhaifu kama vijiti na majani ya miti yanayo chukuliwa na maji ya mvua. Na huko ni kuteketea na kupotelea mbali na rehema kwa madhaalimu kwa ukafiri wao na uasi wao.