Hali kadhaalika Mwenyezi Mungu alichukua ahadi kwa Wakristo, ambao wamesema: Sisi ni Manasara, kwa kuwa wataiamini Injili, na watamuamini Mwenyezi Mungu Mmoja. Nao wakaacha mengi walio amrishwa katika Injili. Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa hayo, kwa kutia uadui na khasama baina ya wao kwa wao, wakawa makundi mbali mbali yenye uadui mpaka Siku ya Kiyama. Na hapo Mwenyezi Mungu atawaambia waliyo kuwa wakiyafanya, na atawalipa kwayo.
Enyi Watu wa Kitabu! Amekujilieni Mtume wetu, Muhammad, akiita watu wafuate Haki. Anakufichulieni mengi mliyo kuwa mkiyaficha katika Taurati na Injili. Na anayaacha mengi katika mliyo yaficha ambayo hayana haja kuyadhihirisha. Amekuleteeni kutoka kwa Mwenyezi Mungu Sharia kaamili, ambayo Sharia hiyo peke yake ni nuru, na inabainishwa na Kitabu kilicho wazi.
Mwenyezi Mungu kwa Kitabu hichi anawaongoa kwenye njia ya uwokofu wanao elekea kutaka radhi zake, na anawatoa kwenye giza la ukafiri kuendea mwangaza wa Imani kwa tawfiki yake, na anawaongoza kwenye njia ya Haki.
Hakika wamekufuru wale wanao dai ati Mwenyezi Mungu ndiye Masihi mwana wa Maryamu!! Ewe Mtume! Waambie hao wanao thubutu kuchezea cheo cha Ungu: Hapana ye yote anaye weza kuzuia matakwa ya Mwenyezi Mungu akitaka kumteketeza Isa na mama yake, na kuwahiliki wote waliomo katika ardhi. Kwani ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yao ni wa Mwenyezi Mungu peke yake. Yeye huumba mfano autakao. Na Mwenyezi Mungu ana uweza mkubwa kabisa. Hashindwi na kitu.