Enyi Waumini! Mwenyezi Mungu amekuharimisheni kula nyamafu, yaani aliye kufa bila ya kuchinjwa kisharia. Na damu inayo tiririka, na nyama ya nguruwe, na yule ambaye wakati wa kuchinjwa ametajiwa jina lisilo kuwa la Mwenyezi Mungu, na aliye kufa kwa kunyongwa, au aliye pigwa mpaka akafa, au aliye kufa kwa kuanguka, au kwa kupigwa pembe, au kwa kuliwa na mnyama mwingine. Ama yule mnaye mdiriki angali yu hai naye ni mnyama wa halali kuliwa, mkamchinja, basi huyo ni halali kwenu. Mwenyezi Mungu ameharimisha kula wanyama walio tolewa sadaka au mhanga kwa masanamu. Na pia ameharimisha kuagua yaliyo ghaibu kwa uganga wa kupiga ramli, na mfano wa hayo. Kula chochote katika vilivyo tajwa kuwa ni haramu ni dhambi kubwa, na ni kutoka kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu. Tangu sasa tamaa ya makafiri kuiviza Dini yenu imekwisha potea. Basi msiwaogope kuwa watakushindeni, bali ogopeni kutofuata amri zangu. Leo nimekukamilishieni hukumu za Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu kwa kukupeni nguvu na kukuimarisheni, na nimekukhitarieni UISLAMU uwe ndiyo Dini. Lakini mwenye kulazimika kwa njaa akala kidogo katika hivyo vilivyo harimishwa, akala ili asife, bila ya kukusudia uasi, basi Mwenyezi Mungu humsamehe mtu huyo kwa kulazimika kula cha haramu asije akafa. Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma na rehema kwa alivyo halalisha. Hafi mnyama wenyewe ila kwa maradhi, na hayo maradhi humdhuru mwanaadamu akila nyama yake, na huenda maradhi mengine yakawa ya kuambukiza. Katika damu vimo vijidudu vya maradhi. Ama katika nyama ya nguruwe mna vitu kadhaa wa kadhaa vya kumdhuru mtu. Na vilivyo chinjwa kwa jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu, na walio chinjiwa masanamu au mashetani, hayo ni mambo ya ibada potovu. Na vilivyo nyongeka, na vilivyo anguka, na kupigwa pembe ni sawa na mfu, au mzoga, kwa kuwa vimekufa kwa vifo vibaya, na khasa kwa kuwa damu yake haikutoka imevilia humo humo.
Ewe Mtume! Waumini wanakuuliza nini walicho halalishiwa katika vyakula na vyenginevyo? Waambie: Mwenyezi Mungu amekuhalalishieni kila chema kipendacho nafsi njema. Na pia amekuhalalishieni kula kinacho windwa na wanyama wenu mlio wafunza kuwinda, kwa kutokana na alivyo kufunzeni Mwenyezi Mungu. Basi kuleni wanacho winda wanyama hao mlio watuma, na mtaje jina la Mwenyezi Mungu pale mnapo watomeza. Na mcheni Mwenyezi Mungu kwa kuzishika sharia zake, wala msikiuke mipaka yake. Tahadharini kumkhalifu Mwenyezi Mungu katika hayo, kwani Yeye ni Mwepesi wa kuhisabu.
Leo, yaani tangu kuteremka Aya hii, mmehalalishiwa kila kilicho chema kipendacho nafsi njema; na pia mmehalalishiwa chakula cha Watu wa Kitabu (Mayahudi na Wakristo), na walio chinja wao, katika vitu ambavyo havikutajwa kuwa ni haramu, kama ilivyo kuwa wao ni halali kwao kula chakula chenu. Na mmehalalishiwa nyinyi kuwaoa wanawake wema wa Kiislamu na wa Ahlil Kitaab (Mayahudi na Wakristo). Hayo kwa sharti mkiwapa mahari yao kwa kusudi ya kuwaoa, sio kwa kuingiana nao kinyume na sharia kwa jahara au kwa kuwaweka mahawara kinyumba. Na mwenye kuipinga Dini, basi amepoteza malipo ya a'mali yake aliyo dhani kuwa ndiyo itamkaribisha, naye huko Akhera ni katika walio hiliki.