Enyi mlio amini! Si halali kwenu kuwachukua Mayahudi na Wakristo mkawafanya ndio marafiki zenu. Wao hao ni sawa sawa katika kukufanyieni uadui. Na mwenye kufanya urafiki nao, basi ni kundi moja nao. Na hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi wanao jidhulumu nafsi zao kwa kufanya urafiki na makafiri.
Ilivyo kuwa kuwafanya hao marafiki hawafanyi ila walio dhulumu, basi utaona kuwa wanao wafanya makafiri ndio rafiki zao wana maradhi katika nyoyo zao, maradhi ya udhoofu na unaafiki. Wao husema: Tunaogopa usije kutupata msiba kwa kugeuka mambo na wao wasitusaidie! A'saa, huenda, Mwenyezi Mungu akamletea Mtume wake kufunguka mambo, na Waislamu wakawashinda maadui zao, au ukadhihiri unaafiki wa hao wanaafiki, wakaamkia majuto, wakijuta kwa zile kufuru na shaka shaka walizo kuwa wakizificha katika nafsi zao.
Na hapo tena Waumini wa kweli watasema kuwastaajabia wanaafiki: Ndio hawa walio kula yamini kwa viapo vya kupita kiasi kwa jina la Mwenyezi Mungu, ya kwamba wao ni wenzenu katika Dini, wenye kuamini kama nyinyi? Wamesema uwongo! Na vitendo vyao vimefisidika, wakawa wamekosa Imani na nusura kutokana na Waumini.
Enyi mlio amini! Mwenye kurejea ukafirini katika nyinyi, baada ya kuamini, hamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Yeye ametukuka na hayo. Badala yao ataleta kaumu iliyo bora kuliko hao, na wao hao Mwenyezi Mungu atawapenda, na atawafikisha kwenye uwongofu, na ut'iifu. Na wao watampenda Mwenyezi Mungu, kwa hivyo watamt'ii. Nao watakuwa na unyenyekevu na huruma kwa ndugu zao Waumini, na watakuwa wakali na wenye nguvu mbele ya maadui zao makafiri. Watapigana jihadi kwa njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama yoyote ya mwenye kulaumu! Hiyo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu humpa amtakaye anaye muwafikia kheri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa fadhila kwa anaye stahiki.
Enyi Waumini! Urafiki wenu nyinyi uwe na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na nyinyi kwa nyinyi katika wanao shika Swala, na wanatoa Zaka, nao wananyenyekea.
Na mwenye kufanya urafiki na Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Waumini na wakawa hao ndio wa kuwategemea kwa msaada na nusura, basi huyo atakuwa katika Hizbu (yaani kundi) ya Mwenyezi Mungu, na Hizbu ya Mwenyezi Mungu ndio yenye kushinda na kufuzu.
Enyi mlio amini! Msiwafanye maadui wa Uislamu walio ifanyia maskhara Dini yenu wakaichezea - nao ni Mayahudi na Wakristo na washirikina, kuwa ndio wasaidizi, wala msifanye urafiki nao. Na mkhofuni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni wakweli katika Imani yenu.