Kila mwenye kuleta wema katika dunia, nayo ni Imani na usafi wa ut'iifu, atapata huko Akhera thawabu kubwa kabisa kwa ajili ya aliyo yatanguliza. Na wenye mema haya watasalimika na khofu na kufazaika Siku ya Kiyama.
Na kila mwenye kuleta uovu katika dunia - nao ni shirki na maasia - na akafa na hayo, basi malipo ya kundi hili ni kuwa Mwenyezi Mungu atawasukumiza juu ya nyuso zao katika Moto, na wataambiwa hapo kwa kuwatahayarisha: Hakika hii leo hamlipwi ila kwa sababu ya shirki yenu na maasi yenu.
Ewe Mtume! Waambie watu: Sikuamrishwa nimuabudu yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa mji wa Makka aliye utukuza, na akaufanya mtakatifu wenye amani, usio faa kumwagwa damu ndani yake, wala kuwindwa wanyama wake, wala kukatwa miti yake. Na vitu vyote viliomo ulimwenguni ni vya Mwenyezi Mungu kuvimiliki na kuvitawala, na mimi nimeamrishwa niwe katika wanao mnyenyekea Mwenyezi Mungu.
Na nimeamrishwa nidumishe kuisoma Qur'ani, kwa ibada, na kuzingatia, na kuwaitia watu wafuate yaliomo humo. Basi mwenye kuongoka, akaiamini, na akakufuata wewe, basi kheri ya hayo na malipo yake ni kwa nafsi yake. Na mwenye kupotea asiifuate Haki, na asikufuate wewe, mwambie: Hakika mimi ni Mtume, naonya, na nafikisha Ujumbe tu.
Na sema, ewe Mtume: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu kwa neema ya Unabii na Uwongofu. Mwenyezi Mungu atakuonyesheni hapa duniani athari za uwezo wake, na Akhera atakuonyesheni ukweli wa aliyo kwambieni, na mtayajua vilivyo. Wala Mwenyezi Mungu hashindwi kukuhisabieni wala haghafiliki na vitendo vyenu.