Hakika mimi nimewaona watu wa Sabai wanatawaliwa na mwanamke, na amepewa kila kheri za kidunia, naye ana kiti cha enzi kikubwa kinacho onyesha dalili ya utukufu wa ufalme na nguvu za madaraka yake.
Nimemwona yeye na watu wake wanaabudu jua, wala hawamuabudu Mwenyezi Mungu. Na Shetani amewazainishia vitendo vyao na wenyewe wakaviona ni vizuri na hali ni viovu. Kwa hivyo amewapoteza Njia ya Haki, basi hawakuongoka.
Hawamsujudii Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye ndiye anayafichua yaliyo fichika katika mbingu na ardhi, na anajua mnayo fanya kwa siri na kwa dhaahiri.
Nenda na barua yangu hii umfikishie yeye na kaumu yake. Kisha jitenge nao ujifiche pahali karibu, uangalie wanarejesheana maneno gani.
Barua ikamfikia yule Malkia, naye basi akawakusanya wahishimiwa wa kaumu yake, na halmashauri wake. Naye akasema: Enyi wahishimiwa! Mimi hakika imenifikilia barua yenye shani kuu.
Kisha akawasomea hiyo barua, nayo imeanzia kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwenye utukufu na neema zote, ambaye daima anawamiminia waja wake rehema zake.
Akaiambia baraza ya washauri wake: Nibainishieni lifaalo katika haya mambo muhimu nilio wekewa mbele yangu. Kwani mimi sikati shauri juu ya jambo lolote mpaka muwe nyinyi mmehudhuria.
Wakamwambia nao wametua: Sisi ni watu wenye nguvu za mwili, na tuna moyo na mashujaa. Hatuogopi vita. Basi angalia wewe jambo unalo taka kutuamrisha nasi ni wenye kut'ii.
Akasema kwa taratibu na kupendelea salama: Hakika watawala wakiingia katika miji mikubwa pamoja na majeshi yao huifisidi, wakaondoa matengenezo yake, wakateketeza makulima na roho, na wakawafanya walio watukufu katika watu wa hiyo miji kuwa ndio madhalili, na huo ndio mtindo wao daima.
Na mimi kwa kupendelea salama na uzima nitampelekea zawadi Sulaiman na kaumu yake, na nitatazama wajumbe watarejea na nini - wataikubali zawadi au watairudisha?