Haikuwa jawabu ya watu wake alipo wakataza ila ni kusema: Mtoleeni mbali Luut'i na wafwasi wake katika mji huu. Kwani wao wanajitakasa hawataki kushirikiana nasi katika haya tuyatendayo.
Basi Sisi tukamwokoa yeye na ahali zake na ile adhabu walio pelekewa wale watu, isipo kuwa mkewe. Mwenyezi Mungu alimkadiria awe na walio baki nyuma ili apate kuangamia kwa adhabu pamoja na makafiri.
Na Sisi tukawanyeshea mvua hao mafisadi, mvua ya adhabu na nakama. Ilikuwa mvua ya kuwahiliki walio onywa kuwa watapata adhabu chungu, na wala wasisikie.
Ewe Mtume! Sema: Hakika mimi namhimidi Mwenyezi Mungu na namsifu Yeye peke yake. Na namwomba Mwenyezi Mungu salama na maamkio kwa waja wake alio wateuwa kwa kuwapa Ujumbe wake. Na ewe Mtume! Waambie washirikina: Je! Kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja, Aliye Mpweke, ni bora kwa mwenye kuamini, au kuabudu masanamu mnayo mshirikisha naye, nayo hayawezi kukudhuruni wala kukufaeni?
Bali, ewe Mtume, waulize: Ni nani aliye ziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yake, na akakuteremshieni kutoka mbinguni mvua yenye manufaa, na kwa hiyo akakuotesheeni bustani nzuri zenye kupendeza. Msingeli weza nyinyi kuiotesha miti yake ya namna mbali mbali, na rangi mbali mbali, na matunda mbali mbali! Mipango hii iliyo umana sawa katika uumbaji inathibitisha kuwa hapana mungu pamoja na Mwenyezi Mungu. Lakini makafiri ni watu walio potoka wakaiacha Haki na Imani, na wameelekea kwenye upotovu na ushirikina.
Bali waulize, ewe Mtume: Nani aliye itengeneza ardhi hata ikafaa kukaliwa na watu wakatulia humo, na akaumba mito kati yake, na juu yake akaumba milima kuizuilia isiyumbe yumbe, na akayatenganisha maji matamu na maji ya chumvi hata yasichanganyike? Hapana mungu pamoja na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mwenye kuumba peke yake. Lakini wengi wa watu hawanafiiki na ujuzi wa Haki kama ilivyo. Wamekuwa kama kwamba hawajui kitu.
Bali waulize, ewe Mtume: Nani anaye muitikia aliye shikwa na shida katika maombi yake, pale anapo shikwa na shida, akamtegemea Mwenyezi Mungu kwa unyonge na unyenyekevu, naye akamwondolea huyo mtu karaha iliyo msibu, na akakufanyeni warithi wa walio kutangulieni katika nchi? Hapana mungu pamoja na Mwenyezi Mungu wa kukupeni neema zote hizi. Lakini nyinyi makafiri, ni kuchache kabisa kuwaidhika kwenu.
Bali waulize, ewe Mtume: Nani anaye waongoza katika nyendo za katika giza la usiku katika safari za nchi kavu na baharini? Na nani anaye zipeleka pepo zinazo bashiria mvua, nayo ni rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu anaye fanya hayo? Mwenyezi Mungu Subhanahu ametakasika kuwa na mshirika.