Na nini cha kutuzuia tusimsadiki Mwenyezi Mungu peke yake, na Haki iliyo teremka kwa Muhammad? Na hali sisi tunamtaraji Mwenyezi Mungu atuingize Peponi pamoja na watu wenye Imani njema na vitendo vyema.
Kwa hivyo Mwenyezi Mungu amewaandikia malipo kwa vile kuungama kwao, nayo ni Bustani yenye kupita mito chini ya miti yake, na majumba ya fakhari ya kukaa humo daima, pamoja na watu ambao ni njema itikadi zao na vitendo vyao.
Na walio mpinga Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wakazikanya dalili alizo wateremshia kuwa ni uwongofu wa kufikia Haki, ni wao peke yao wanao stahiki adhabu kali katika Jahannamu.
Enyi mlio amini! Msijiharimishie nafsi zenu vitu vizuri alivyo kuhalalishieni Mwenyezi Mungu, wala msipite mipaka aliyo kuwekeeni Mwenyezi Mungu ya kufuata mambo ya wastani. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi watu wanao pindukia mipaka.
Na kuleni vitu alivyo kupeni Mwenyezi Mungu na akavifanya vyepesi kwenu, na akavifanya ni halali na ni vizuri kwa nafsi zenu. Na daima mwogopeni Mwenyezi Mungu, na mt'iini Yeye maadamu nyinyi mnamuamini Yeye.
Mwenyezi Mungu hakutiini adabu kwa sababu ya kuapa kiapo msicho kusudia. Bali hakika Yeye hukutieni adabu kwa sababu ya kuvunja viapo mlivyo vikusudia na yamini mliyo jifunga nayo. Basi ikiwa mmevunja kiapo itakupaseni mfanye jambo la kukughufirieni dhambi zake. Na mambo yenyewe ni: kuwalisha mafakiri kumi kwa siku moja, kwa chakula cha kawaida mnacho kila nyinyi na jamaa zenu mnao waangalia, yaani watu wenu wa nyumbani bila ya israfu wala ubakhili. Au kuwavika mafakiri kumi kwa kivazi kilicho zowewa. Au kumkomboa mtu kutoka utumwani. (Na mfano wa mtumwa ni mtu alioko kifungoni kwa dhulma, au chini ya utawala wa dhulma.) Ikiwa mwenye kuapa hawezi kutenda lolote katika hayo, basi itampasa afunge siku tatu. Na kila moja katika mambo haya hufuta dhambi za mwenye kuapa kiapo cha kutilia niya na akakivunja. Nanyi zilindeni yamini zenu, msiape katika mambo yasiyo kuwa laiki yake, na wala msiache kutenda kitendo cha kughufiria dhambi pindi mkivunja kiapo. Kwa mpango huu Mwenyezi Mungu anakufafanulieni hukumu zake ili mpate kushukuru neema zake kwa kuzijua na kuzifuata vilivyo. Katika hukumu ya yamini pana mawili yafaa tuyazingatie. Kwanza: Uislamu umeraghibisha sana kukomboa watumwa. Sababu nyingi zinazo wajibisha hayo. Kafara nyingi za dhambi zinahitaji kukomboa. Kafara ya kula mchana Ramadhani yahitaji ukombozi, n.k. Na katika hayo yanaonyesha Uislamu unachukia utumwa. Uislamu uliukiri utumwa kwa kuwa maadui wao walikuwa wakiwatia utumwani Waislamu, basi na Uislamu ukaruhusu kuwatendea wao vivyo hivyo. Pili: Uislamu unakazania kulisha masikini kila ikipatikana fursa.
Enyi wenye kumsadiki Mwenyezi Mungu na Vitabu vyake na Mitume wake, wenye kuifuata Haki! Kunywa au kuvuta chochote kinacho lewesha, kucheza kamari, na kusimamisha mawe ya kutolea mihanga kwa ajili ya masanamu mnayo yaabudu, na kuagua kwa mishale, na mawe, na karatasi za kuagulia kudra iliyo ghaibu...yote hayo si chochote ila ni uchafu wa kiroho, na upotovu. Na hayo ni kupambiwa na Shetani tu. Basi yaachilieni mbali ili mpate kufuzu duniani kwa maisha bora, na Akhera mpate Janna yenye neema. Kuagua kwa mishale: ilikuwa ikiandikwa juu ya vijiti, kimoja kiliandikwa: "Mola wangu Mlezi kaniamuru", na kingine:"Mola wangu Mlezi kanikataza", na kingine hakikuandikwa kitu. Hutiwa vijiti hivyo katika mfuko kisha huchanganywa, na kohani hutia mkono wake akachomoa kimojapo, na akamjuvya mwenye kuuliza lilio aguliwa