Mke wa Ibrahim alipiga ukelele kwa kustaajabu: Ajabu gani hii, jamani! Nizae mimi kikongwe, na huyu mume wangu mnamuona kesha kuwa kizee kabisa! Kama huyu hapati mwana tena. Hakika haya ninayo yasikia ni mambo ya ajabu. Vipi vikongwe viwili kama mimi na mume wangu wazae tena?
Malaika wakamwambia: Unastaajabu nyinyi wawili kupata mwana kwa ajili ya uzee wenu? Haya yanatokana na amri ya Mwenyezi Mungu asiye shindwa na chochote. Hiyo ndiyo rehema ya Mwenyezi Mungu. Na neema zake ni nyingi juu yenu wa ukoo wa Nabii. Basi hapana la ajabu nyinyi kupewa wasio pewa wenginewe. Mwenye kutenda hayo hakika anastahiki kuhimidiwa, ni mwingi wa hisani na ukarimu na upaji.
Zilipo mtoka khofu Ibrahim, na akaisikia bishara ya kumfurahisha ya kupata mwana, ikamwingia huruma, akaanza kujadiliana na wale wajumbe katika shauri la kuangamizwa kaumu Lut'.
Hakika Ibrahim ni mpole mno, hapendelei mapatilizo ya kwa haraka, mwingi wa kuungulika na kuona uchungu kwa shida zinao wapata watu, tena yeye ni mwenye kutubu na kurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa yale ayapendayo na kuyaridhi. Basi ule upole wake, na rehema zake, na huruma zake ndizo zilizo mpelekea kubishana kule kwa kutaraji kuwa asaa Mwenyezi Mungu akawaondolea adhabu watu wa Lut', na wao wapate kutubu na kurejea kwake.
Malaika wakasema: Ewe Ibrahim! Wachilia mbali haya majadiliano, na kuwatakia rehema watu hawa. Kwani amri ya Mola wako Mlezi ya kuwaangamiza imekwisha kuja! Hapana budi kuwa adhabu itawashukia, na wala haitarudishwa kwa majadiliano au bila ya majadiliano.
Walipo kuja wajumbe wetu, hao Malaika, kwa Lut' kwa sura ya vijana wazuri, Lut' aliungulika na akaudhika. Alihisi unyonge hana nguvu za kuwahami na hao watu wake, akawaonea dhiki kwa kuwaogopea ufisadi wa kaumu yake! Akasema: Hii leo ni siku ya karaha kubwa na machungu!
Watu wake wakajua kuwa wamekuja wale wageni, wakamwendea mbio mbio. Na kabla ya hayo ilikuwa kazi yao kufanya huo uchafu wao na kutenda maovu! Lut' akawaambia: Enyi watu wangu! Hawa binti zangu, waoeni. Hao ni safi zaidi kwenu kuliko kwenda kufanya uchafu kwa wanaume! Mwogopeni Mwenyezi Mungu, na jilindeni nafsi zenu na adhabu yake; na msinifedhehi na mkanidharaulisha kwa kuwavamia wageni wangu! Basi hivyo hamna kati yenu hata mtu mmoja mwenye rai iliyo sawa, mwenye akili iliyo ongoka, akakuzuieni na maasi na akakukatazeni maovu?
Wakasema: Wajua vyema ewe Lut', kuwa sisi hatuna haki ya kuwaoa binti zako, wala hatuwataki. Na wewe hapana shaka unajua tukitakacho tulipo kujia kwa haraka.
Lut' akasema: Laiti ningeli kuwa nina nguvu au nina nguzo yenye nguvu ya kutegemea, msimamo wangu juu yenu ungeli kuwa mwengine, na ningeli weza kuwalinda wageni wangu nikakuzueni msiwafanye mambo mabaya.
Malaika wale wakamwambia, na wao ukweli wao ulikwisha dhihiri: Ewe Lut'! Usikhofu wala usihuzunike! Sisi ni wajumbe wa Mola wako Mlezi, wala si binaadamu kama tuonekanavyo kwako na kwa hawa kaumu yako. Wala wao hawa hawatakufikishia shari yoyote ya kukuudhi au kukudhuru. Basi toka wewe na ahali zako usiku ukisha zagaa. Mtoke mji huu, wala yeyote katika nyinyi asigeuke kutazama nyuma, asije akaona vitisho vya adhabu naye akasibiwa na shari yake! Lakini mkeo ambaye amekukhuni, yeye hatokuwa pamoja na watao toka nawe. Yeye lazima yampate yatao wapata hawa watu. Na miadi ya kuangamia kwao ni asubuhi, na miadi hiyo ni karibu. Basi usitie khofu.