Na subira haipelekei ila kwenye kheri na kufanikiwa kote kuwili, duniani na Akhera. Basi msikae nyuma mkaacha kwenda kupigana Jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Wala msiogope kufa katika Jihadi, kwani mwenye kufa katika Jihadi huyo si maiti, hakufa, bali yuhai maisha ya juu kabisa, ijapo kuwa hawa tunao waona wahai hawatambui hayo.
Subira ni ngao na silaha ya Muumini ambayo kwayo hushindia kila shida na mashaka. Na nyinyi zitakuja kupateni shida nyingi. Tutakujaribuni na kukufanyieni mitihani kwa vitisho vya maadui, kwa njaa, na uchache wa vifaa, na kupungukiwa mali, na watu kufa, na kupotea mazao. Na hapana la kukulindeni katika mtihani huu mkali ila Subira. Basi Ewe Nabii! Wape bishara nzuri wanao subiri kwa moyo na ulimi.
Wale ambao kwamba yanapo wateremkia machungu ya kuwaumiza wanaamini ya kuwa hakika kheri yote na shari inatokana na mwenyewe Mwenyezi Mungu, na ya kwamba amri yote ni ya Mwenyezi Mungu. Hao husema: Sisi ni milki ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na sisi ni wenye kurejea kwake Yeye. Sisi hatuna letu jambo lolote. Na Yeye ni mwenye kustahiki kushukuriwa kwa anacho toa, na juu yetu kusubiri wakati wa kujaribiwa, na kwake Yeye ndiyo zipo thawabu na malipo.
Basi hao wenye kusubiri, wenye kumuamini Mwenyezi Mungu, wanapewa bishara njema kuwa watapata maghfira na ihsani ya Mwenyezi Mungu, na wao ndio wenye kuongoka njia ya kheri na uwongozi mwema.
Na kama alivyo kuwa Mwenyezi Mungu ametukuza hadhi ya Alkaaba akaifanya iwe ndiyo Kibla cha Swala, hali kadhaalika ametukuza shani ya vilima viwili viliopo Makka, navyo ni Safaa na Marwa, akavifanya miongoni mwa mahala pa kufanyia ibada ya Hijja. Basi imewajibikia baada ya kuizunguka Alkaaba kwa kut'ufu, kwenda huku na huku baina ya vilima viwili hivyo mara saba. Kwenda huko kunaitwa Sa'yu. Na baadhi yenu labda walikuwa wakiona vibaya kufanya hivyo kwa kuwa kilikuwa kitendo cha siku za jahiliya kabla ya kuja Uislamu. Lakini kweli iliopo ni kuwa hiyo ni ada ya Kiislamu ya tangu zamani. Basi hapana ubaya wowote kufanya Sa'yu baina ya vilima viwili hivi kwa mwenye kunuwiya Hijja na Umra. Na Muumini na afanye jambo la kheri kama awezavyo, kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa ayatendayo, na Yeye atamlipa kwa a'mali yake.
Hao wanao kukatalieni Dini yenu wako makundi mawili: kundi moja ni katika Watu wa Kitabu wanao ijua Kweli, lakini wanaificha kwa kujua na kwa inda. Na kundi jengine ni la washirikina ambao nyoyo zao ni pofu, kwa hivyo hawaioni Kweli, na badala ya Mwenyezi Mungu Mmoja wakawa wanaabudu miungu myengineo. Basi Watu wa Kitabu walio jua ushahidi wa ukweli wako wanajua haki ya Dini yako, lakini kisha wanazificha hizo dalili ili watu wasijue. Mwenyezi Mungu atawapatiliza ghadhabu yake, na atawaepusha rehema yake, na kila wanao omba katika Malaika, na Wanaadamu na Majini watawaapiza wasipate rehema ya Mwenyezi Mungu.
Wala hapana atakaye vuka na laana hiyo katika wao ila aliye tubu na akatenda mema kwa kuacha kuficha Haki, akayadhihirisha aliyo kuwa akiyaficha katika sifa za Mtume na Uislamu. Mwenyezi Mungu atakubali toba yake na atamfutia dhambi zake, kwani Yeye ndiye anaye kubali toba ya waja wake kwa huruma na rehema yake.
Ama wale walio kakamia na ukafiri, na wakafa bila ya toba wala majuto, jaza yao ni laana ya Mwenyezi Mungu, na Malaika na watu wote.
Na wataendelea katika laana hii na katika Moto, wala hawatapunguziwa adhabu, wala hawatapewa muhula wala haitoakhirishwa. Hata wakiomba muhula na kuakhirishwa hawataitikiwa.
Hakika Mungu wenu anaye stahiki kuabudiwa pekee ni Mmoja. Hakuna mungu mwenginewe, wala hapana utawala ila wake. Tena Yeye amesifika kuwa ni Mwenye rehema, basi Yeye ni Rahim, Mwenye Kuwarehemu waja wake katika kuwaumba na kuwafanya walivyo.