Hakika wale wachache wa akili walio potezwa na pumbao lao wasiweza kufikiri sawa na kuzingatia miongoni mwa Mayahudi, na Wakristo, na washirikina na wanaafiki, watachukizwa kuwaona Waumini wameacha kukielekea kibla cha Beitul Muqaddas (Yerusalemu) walicho kuwa wakikielekea kwanza katika Sala. Na wao wakiona kuwa hicho kinastahiki zaidi kuliko kibla kingine, yaani cha Alkaaba. Basi waambie, Ewe Nabii! Jiha zote ni za Mwenyezi Mungu. Hapana upande ulio bora kuliko mwengine kwa dhati yake, lakini Mwenyezi Mungu ndiye mwenyewe anachagua upande autakao uwe ni kibla cha Sala. Na Yeye kwa mapenzi yake huuongoa kila umma katika wanaadamu kufuata njia iliyo sawa anayo ikhiari Yeye na anayo ikhusisha Yeye. Na sasa umekuja Ujumbe wa Muhammad unafuta risala zote zilizo tangulia, na Kibla cha sasa cha Haki ni hichi cha Alkaaba iliyopo Makka.
Na kwa ajili ya kutaka huku ndio tukakuongoeni kwenye Njia Iliyo Nyooka kabisa, na tukakujaalieni muwe Umma wa katikati ulio bora kwa muujibu tulivyo iwafikisha Dini sahihi na vitendo vyema, ili muwe wenye kuthibitisha Haki kwa mnasaba wa sharia zilizo tangulia, na ili Mtume awe mlinzi juu yenu, akikupeni nguvu kwa uwongozi wake kwa muda wa uhai wake, na kwa kufuata njia yake na mwendo wake baada ya kufa kwake. Ama kibla cha Beitul Muqaddas tulicho amrisha kifuatwe kwa muda fulani tulikifanya kuwa ni mtihani kwa Waislamu ili watambulikane wanao t'ii wakielekee kwa ut'iifu, na wenye kuchukuliwa na mori wao wa Kiarabu kwa kufuata nyao za Ibrahim tu waivunje amri ya Mwenyezi Mungu na kwa hivyo wapotelee njia ya upotovu. Na ilikuwa ile amri ya kuelekea Beitul Muqaddas ni katika mambo magumu ila kwa wale ambao wamejaaliwa kupata hidaya ya Mwenyezi Mungu. Ikawa kufuata amri hii miongoni mwa nguzo za Imani. Mwenye kuelekea kibla cha Beitul Muqaddas katika zama ilipo amrishwa hayo hakupoteza Imani yake na ibada yake kwa upole na rehema ya Mwenyezi Mungu.
Na Sisi tulikuona vipi unazichungua mbingu asaa uteremke Wahyi (ufunuo) wa kugeuza Kibla cha Beitul Muqaddas ufuate cha Alkaaba ambacho unakipenda, kwa kuwa ndicho Kibla cha Ibrahim, baba wa Manabii, na baba wa Mayahudi na Waarabu. Na hapo pana Maqaamu Ibrahim, alipokuwa akisimama Ibrahim. Kwa hivyo hichi ni Kibla kilicho kusanya wote, ijapokuwa kinaacha kibla cha Mayahudi. Basi hivi sasa Sisi tunakupa lile ombi lako. Kwa hivyo katika Sala zako elekea Masjidil Haraam (Msikiti Mtakatifu). Na nyinyi Waumini, kadhaalika, elekeeni huko popote pale mlipo. Watu wa Kitabu wanao udhika kwa kukiacha kwenu Kibla cha Beitul Muqaddas wanajua katika vitabu vyao kuwa nyinyi ni watu wa Alkaaba. Na wanajua kuwa amri ya Mwenyezi Mungu inawakhusisha watu wa kila sharia na kibla chao. Na hii ni haki inayo tokana na Mola wao Mlezi. Lakini wao wanataka kukufitinisheni na kukutilieni shaka katika Dini yenu. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika nao, na Yeye atawalipa kwa wayatendayo.
Na hakukua kutoridhika kwao Watu wa Kitabu nanyi ni kwa kudanganyikiwa ambako kwaweza kuondoka kwa hoja, bali kuudhika huko ni kwa inadi na kiburi. Kwa hivyo Ewe Mtume! Hata ukiwaletea kila hoja ya kukata kuwa Kibla chako ndicho cha kweli, hawakubali kukifuata Kibla chako. Ikiwa Mayahudi wangali wanatumai kuwa bado utarejea kwenye kibla chao, na wanatoa hiyo ni shuruti ya kusilimu kwao, basi watavunjika moyo, wala wewe hutofuata kibla chao. Na hao watu wa Kitabu kila kikundi chao kina kibla chake mbali. Wakristo hawafuati kibla cha Mayahudi, wala Mayahudi hawafuati kibla cha Wakristo, na kila mmoja kati yao anawaona wengine hawamo katika haki. Basi wewe thibiti hapo hapo kwenye Kibla chako, wala usiyaendekeze matamanio yao. Kwani mwenye kuyafuata matamanio yao baada ya kwisha pata ujuzi kuwa wao ni wapotovu, na kujua kuwa yeye yuko katika haki, basi huyo ni katika walio dhulumu na wenye kubobea katika dhulma. Wanasema wafasiri kuwa Mayahudi wanaelekea kwenye Mwamba katika Beitul Muqaddas na Wakristo wanaelekea Mashariki.