Mwenyezi Mungu ameijibu kauli ya Mayahudi walipo sema kwamba Wana wa Israili hawakupata kwenda kinyume na Haki. Alisema: Ewe Nabii! Wakumbushe pale tulipo unyanyua mlima juu ya Wana wa Israili ukawa kama kiwingu, na wakafazaika kwa kuwa walidhani utawaangukia. Nasi tukawaambia wakati ule ulipo nyanyuliwa na wao wamo katika khofu: Yashikeni ya uwongofu tuliyo kupeni katika Taurati kwa nguvu na kuazimia ut'iifu. Na kumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate kuzingatia na zitengenee nafsi zenu kwa kuchamngu.
Hapa Mwenyezi Mungu amebainisha hidaya ya wanaadamu kwa kusimamisha dalili katika viumbe, baada ya kwisha bainisha kwa njia za Mitume na Vitabu. Alisema: Ewe Nabii! Waambie watu pale Mola wako Mlezi alipo watoa kutoka migongo ya wanaadamu na watoto wao na wanao zaliwa karne baada ya karne, kisha akwasimamishia dalili za Ungu wake, na akawapa akili na nadhari ya kuwawezesha kuzijua, na kwa hizo akili na nadhari waweze kutambua Tawhidi na Rubuubiya, yaani kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja Pekee na ni Mola Mlezi wa viumbe vyote, hata wakawa hao wanaadamu kama walio ulizwa: Je, Mimi siye Mola wenu Mlezi? Nao wakajibu: Kwani, Wewe ndiye Mola Mlezi wetu. Tunajishuhudia hayo juu ya nafsi zetu...Haya ni kwa kuwa kumkini kwao kupata kujua hizo hoja na dalili, na kutamakani kwao katika hayo imekuwa kama kwamba ni kukiri na kuungama. Na Sisi tumefanya haya ili msije kusema Siku ya Kiyama: Hakika sisi tulikuwa tumeghafilika na hiyo Tawhidi, na tulikuwa hatuijui. Katika Aya hii inaonyesha kuwa watoto asili yake wanatoka kwenye uti wa mgongo. Na ilimu ya kisasa imethibitisha kuwa kokwa za khaswa zinakuwa katika sehemu ya mgongo chini ya mafigo. Na zinakaa hapa mpaka katika miezi ya mwisho ya mimba ndio huteremka pale pahali pake pa kawaida panapo onekana. Na pengine hata hivyo huchelewa kuteremka hata baada ya mtoto kuzaliwa. Kadhaalika mayai ya mwanamke yanafanyika chini ya figo khasa, kisha ndio huteremka pahala pake karibu na tumbo la uzazi.
Au mtasema: Walishiriki baba zetu kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tumewafuata tu. Basi ewe Mola Mlezi wetu! Unatushika utuhiliki kwa walio yafanya wapotovu miongoni mwa baba zetu, kwa kujenga misingi ya ushirikina tulio endelea nao? Basi hamna hoja.
Kwa mfano wa maelezo wazi yenye hikima tunawabainishia wanaadamu dalili za kuwepo Mwenyezi Mungu, ili warejee waache ukhalifu wao na kuwafuata wapotovu.
Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa wanao kadhibisha kwa Aya zake alizomteremshia Mtume wake. Akasema: Ewe Nabii! Wasomee kaumu yako khabari za mtu mmoja katika Wana wa Israili. Tulimpa ilimu ya kuzijua Ishara tulizo wateremshia Mitume wetu. Yeye huyo akazipuuza, wala asizishughulikie. Basi Shetani akamfuata kwa khatua zake, na akamtawala kwa upotovu wake, akawa katika kundi la walio potea.
Na lau tungeli taka kumnyanyua afike daraja za watu wema, tungeli mnyanyua kwa kumwezesha kuyatenda maamrisho ya hizo Aya.. Lakini yeye alishikamana na dunia, na hakuweza kunyanyuka kwendea uwingu wa uwongofu. Akafuata matamanio yake. Akawa hali yake daima yumo katika dhiki, na kushughulika kwake ni kwa dunia, na tafakuri zake duniani ni kutaka kuipata hiyo dunia basi. Hali yake ni kama hali ya mbwa anapo kuwa katika hali ovu kabisa, anavyo kuwa daima anapumua na kutoa limi lake nje, ukimkemea au ukimwacha. Hudorora ulimi wake kwa kuvuta pumzi kwa shida! Kadhaalika mwenye kuipenda dunia hudumu daima katika kuwania starehe zake na matamanio yake! Hakika hizo ndizo sifa zinazo mueleza huyo mwenye kuziacha Aya zetu, na ndio sifa ya wote wanao zikadhibisha Aya zetu zilio teremka. Basi wasimulie kisa chake hichi, huenda wakafikiri na wakaamini.
Ni mbaya kweli hali ya hao wanao zipinga Ishara zetu, na kwa huku kukengeuka kwao na kuacha Haki hakumdhulumu mtu ila nafsi zao tu.
Na yule ambaye Mwenyezi Mungu amemwezesha kufuata njia ya haki huyo basi ndie aliye ongoka kweli, mwenye kupata furaha ya kote kuwili duniani na Akhera. Na mwenye kukosa uwezesho huo kwa sababu ya kumilikiwa na pumbao lake basi watu hao ndio walio khasiri.