Wana wa Israili wakaivuka bahari kwa uangalizi wetu, na kuwaunga mkono na kuwafanyia mepesi mambo yao. Baada ya kwisha vuka waliwakuta kaumu wameshika ibada ya masanamu. Walipoona hivi yale waliyo kuwa wameyazoea kuwaona Wamisri wakiabudu masanamu yaliwaghilibu, wakamtaka Musa awafanyie nao masanamu wayaabudu, kama ilivyo kuwa wale kaumu wana masanamu yao wanayo yaabudu! Hapo hapo Musa a.s. aliwatahayarisha na kuwakanya, akasema: Hakika nyinyi ni watu wapumbavu, msio na akili! Hamjui ibada ya Haki, wala hamumjui Mungu anaye stahiki kuabudiwa!
Hawa mnao waona wanaabudu masanamu, hapana shaka haya walio nayo ni yenye kuangamia, na hii dini waliyo nayo ni potovu , bure bilashi. Na a'mali zao ni zenye kupotea, wala hazibaki.
Je, nikutafutieni wa kuabudiwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa viumbe vyote, na Yeye ndiye aliye kupeni fadhila, na akakupeni neema asio pata kupewa mwengine asiye kuwa nyinyi katika zama zenu?
Kumbukeni alipo kuvueni Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa uangalizi wake na watu wa Firauni, walio kuwa wakikuadhibuni ukomo wa adhabu, wakikudhalilisheni muwatumikie katika kazi ngumu, wala hawakukuoneeni huruma kama wanyama, wakiuwa wavulana wenu na wakiwabakisha wasichana ili mzidi kudhoofika kwa wingi wa wanawake! Na katika adhabu za Firauni zilizo kushukieni, na kukuvueni nazo, pana mtihani mkubwa wa Mola wenu Mlezi, wala hapana mfano wake.
Tulimuahidi Musa tutazungumza naye na tutampa Taurati baada ya kutimia masiku (wingi wa "usiku") thalathini ya yeye kuabudu. Na tukauongeza muda huo kwa masiku kumi, kutimiza ibada. Yakawa masiku arubaini. Musa akamwambia nduguye Haarun alipo kuwa anakwenda kuzungumza na Mwenyezi Mungu: Kuwa badala yangu kwa hawa watu wangu. Na watengenezee mambo yao yanayo hitajia kutengenezwa. Na tahadhari na kufuata njia ya mafisadi. (Angalia: Kwa Kiswahili safi, "Masiku" ni wingi wa "Usiku". Ama wingi wa "Siku" ni "Siku" vile vile kama ilivyo katika aghlabu ya maneno mengine yanayo anzia "S", kama Saa, Sanda, Sahani, Sabuni, Safari, Sufuria n.k.)
Na alipo kuja Musa kuzungumza nasi, na Mola Mlezi wake akanena naye kwa maneno ambayo siyo kama kusema kwetu, Musa alisema: Ewe Mola Mlezi wangu! Nionyeshe dhati yako na unidhihirikie, nipate kukutazama nizidi utukufu. Mwenyezi Mungu akasema: Huwezi kuniona. Kisha Subhanahu, Aliye takasika alitaka kumkinaisha kuwa hawezi kumwona, akamwambia: Walakini utazame huo mlima ambao una nguvu kuliko wewe. Ukithibiti pahala ulipo wakati wa kudhihiri kwangu, basi utaniona nikijidhihirisha kwako. Basi Mola wake Mlezi alipo jionyesha kwa huo mlima kwa njia inayo wafikiana naye Mtukufu, mlima ulivurugika ukawa sawa sawa na ardhi. Musa akaanguka, kazimia kwa kitisho alicho kiona. Alipo zindukana kutokana na kuzimia kwake alisema: Nakutakasa mtakaso mkuu na kuonekana kwako duniani! Hakika mimi ninatubu kwako kuja kukutaka kitu bila ya ruhusa yako. Na mimi ni wa mwanzo katika zama zangu wa wanao amini utukufu wako na ubora wako.