Na pindi ikiwa mnataka kubadili mke pahala pa mke mwengine, na ikawa mmempa mmoja wao mali mengi basi si halali kwenu kuchukua chochote katika hayo. Jee mtachukua hayo kwa njia ya upotovu na kwa dhambi iliyo wazi?
Na vipi ikufalieni nyinyi kutaka kurudishiwa mahari mliyo kwisha yatoa, na hali mlikwisha changanyika nyinyi kwa nyinyi, na wao wanawake wakafungamana nanyi kwa agano lenye nguvu ambalo kwalo Mwenyezi Mungu amewajibisha muingiane nao kwa ndoa.
Wala nyinyi, watoto, msiwaoe wanawake walio wahi kuolewa na baba zenu. Jambo hilo ni uchafu na linachusha, na linakirihiwa na Mwenyezi Mungu na watu. Na hiyo ni njia ovu kabisa. Lakini Mwenyezi Mungu anasamehe yaliyo kwisha tendeka katika zama za ujahili. Waarabu katika zama za ujahili walikuwa na ada zisio mpa heshima mwanamke, bali zikimdhulumu sana, na zikikata makhusiano mema katika ukoo. Ilikuwa mtu akifa baba yake na akawa na wake wasio kuwa mama yake mzazi, akilazimishwa kuwaoa, au akiwarithi wake za baba yake bila ya ndoa mpya. Na ilikuwa mtu akimwacha mke basi humpokonya kwa dhulma na uadui mahari yote aliyo mpa. Na walikuwapo walio kuwa wakimzuia huyo mt'laka asiolewe na mtu mwengine, kwa jeuri na inda. Ukaja Uislamu, ukamlinda mwanamke na dhulma hii iliyo wazi, ukakataza kurithiwa mke, na kumpokonya mahari yake hata chembe, ijapo kuwa ni mali mengi, na ukakataza kumzuia mt'alaka asiolewe, au kumkera ili apate kutaka yeye mke t'alaka kwa kutoa mali. Na katika mtindo wao Waarabu wa jahiliya ilikuwa yafaa mtu kumwoa aliye kuwa mke wa baba yake na akafarikiana naye kwa t'alaka au mfano wake. Uislamu ukakataza hayo, na ukauwita mtindo huo ni uchafu, kwa sababu ni jambo baya analo lichukia Mwenyezi Mungu na kila mwenye akili sawa. Huo ndio uadilifu wa Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu amekuharimishieni kuwaoa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu (ndugu wanawake) na shangazi zenu, na khaalati zenu (mama wadogo) na binti wa ndugu, na binti wa dada, na mama walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wakwe. Na walio harimishwa bila ya kunasibiana kwa damu ni: mama wa kunyonyesha, dada wa kunyonya, mama mkwe, binti za wake kwa waume wengine ikiwa hao wake wameingiliwa, na wake wa watoto mlio wazaa, na kuwaoa pamoja ndugu wawili. Yaliyo pita katika siku za ujahili yamesamehewa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe kwa yaliyo pita kabla ya mpango huu, na Mwenye kuwarehemu katika aliyo kuwekeeni sharia. Ni Sharia ya Kiislamu pekee iliyo harimisha kwa sababu ya kunyonyesha. Anaye nyonya anakula kutokana na mwili wa mnyonyeshaji kama anavyo kula kutokana na mama yake ndani ya tumbo lake. Wote hao wawili wanakuwa ni sehemu yake huyo mtoto. Hapana khitilafu baina ya kukua ndani ya chumba na ndani ya tumbo. Na katika kuharimisha kwa kunyonyesha ni kumtukuza mnyonyeshaji, kwani anakuwa kama mama. Na haya ni kuzidi kushajiisha kunyonyesha kimaumbile, sio kwa chupa, kwa watoto wachanga.